YALIYOJIRI KESI YA NONDO LEO MAHAKAMANI-IRINGA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi la kutoambatanisha kielelezo cha maandishi yaliyotolewa na upande wa Jamhuri katika kesi ya Mwanafunzi Abdul Nondo.

Siku ya Alhamisi ya tarehe 19 April Mwaka huu kesi hiyo iliahirishwa kutokana mvutano wa mawakili wa pande zote mbili juu ya utofauti wa majina ya Mwanafunzi Abdul Nondo yaliyoandikishwa na askari wa mapokezi pamoja na Askari wa upelelezi na kwamba upande wa utetezi ulidai kuwa ni watu wawili tofauti.

Mahakama imefikia uamuzi wa kutupilia mbali pingamizi hilo kutokana na kujiridhisha kuwa mshatakiwa Nondo ndio mhusika kwani Majina yaliyoandikishwa kwa askari wa mwanzo Copro Salumu yalisomeka kuwa Abdul mahmoud Omary Nondo na kwa Askari wa upelelezi Copro John yalisomeka kuwa ni Mahmoud Omary Nondo na hivyo jina moja tu la Abdul ndio lilikuwa limekosekana.


Hakimu wa kesi hiyo John Mpitanjia amesema kuwa maelezo yaliyoandikishwa na askari Polisi yaliandikwa chini ya kifungu cha 34, B section C na kwamba Mahakama inapokea kielelezo chini ya kifungu hicho na sio vinginevyo.

Aidha amesema kuwa majina kutofautiana sio jambo la msingi kwani jina linalokosekana ni moja tu pekee yake la Abdul hivyo Mahakama imeridhia kuwa mshtakiwa ni ndio mhusika wa kesi hiyo.

Katika hatua nyingine Mpitanjia aliamuru kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi ambapo upande wa utetezi chini ya wakili Chance Mloga aliomba kuhairishwa kwa kesi hiyo kutokana na wakili kiongozi Jebrah Kambole kutokuwepo mahakamani hapo.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa serikali Abel Mwandanalamo ulipinga vikali ombi hilo na kuiiomba mahakama kuendelea kusikiliza mashahidi kutokana na gharama ambazo serikali imekuwa ikizitumia kuwahudumia mashahidi hao tangu tarehe 17 mwezi huu.

Mahakama ilikubali ombi hilo na kuamuru mashahidi kuendelea kusikilizwa ambapo shahidi wa Tatu Mwanafunzi kutoka chuo kikuu Dar Es Salaam kitengo cha Sheria mwaka wa nne Paul Emmanuel Kisago mkazi wa Ubungo Dar Es Salaam.

Baada ya Mwanafunzi huyo kutoa ushahidi wake wakili upande utetezi Chance Mloga aliiomba mahakama kutoendelea kusikiliza mashahidi waliobakia na kuomba kuahirisha shauri hilo kutokana na kutojisikia vizuri.

Hakimu Mpitanjia alitoa nafasi ya makubaliano upande wa utetezi na upande wa jamhuri na wakakubaliana kuahirishwa kwa kesi mpaka Jumatano ya Tarehe 25 mwezi huu na Hakimu akahairisha kesi hiyo.

Itakumbukwa kuwa Nondo anatuhumiwa kwa makosa mawili. Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.

Shtaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga.







Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment