WANAWAKE IRINGA WATOA MSAADA KWA WATOTO WENYE MAZINGIRA MAGUMU

Mtoto Amoni Swai akipokea msaada kutoka kwa wanawake Iringa

Mtoto Amina Chande akipokea Msaada wa Sabuni

 Wanawake wakijipanga kutoa msaada kwa watoto wenye mazingira magumu




Na Dajari Mgidange,

Wanawake Mkoani hapa wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa baadhi ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ndani ya manispaa ya Iringa ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuadhimishwa kwa siku ya wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ya tarehe 8 mwezi wa 3.

Msaada huo umetolewa kwa kata 18 zilizopo ndani ya Manispaa ambapo kila kata kupitia watendaji waliweza kuchagua watoto wanne pekee watakaopata mahitaji hayo ikiwa ni sabuni, unga wa ugali, vifaa vya shule na mahitaji mengine mbalimbali.

Suzan Nyagawa ni mratibu kitengo cha wanawake Mkoani Hapa amesema kuwa wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika Mkoani hapa katika viwanja vya Kichangani yaliyohudhuriwa na Mgeni rasmi Mbunge wa Viti Maalumu Iringa kupitia CCM Mhe. Rita Kabati, wanawake wengi waliweza kutoa vitu mbalimbali ambavyo walivikusanya kwaajili ya kutoa kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

“Tumeamua kugawa vitu hivi kwa watoto wanne kila kata kutokana na ufinyu wa vitu vyenyewe vilivyopo”. Amesema Suzan Nyagawa.

Kwa upande wake Dina Kisama ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku ya mwanamke Duniani ndani ya Manispaa amesema kuwa zoezi hilo wanafanya kila mwaka wakati siku ya wanawake inapofika na wanalazimika kama akina mama kujichangisha kwaajili kutoa msaada kwa wasiojiweza.

“Si lazima sana uwe tajiri ndipo uweze kutoa msaada chochote kitu ulicho nacho unaweza toa kwaajili ya wasiojiweza na niombe Taasisi mbalimbali na wadau wote waweze kufanya zoezi hili liwe endelevu lisiwe kila mwaka tu kwani kila siku hawa watoto wenye mazingira magumu wanahitaji misaada tofauti tofauti”. Amesema Kisama.

Naye Diwani wa Viti maalumu kupitia Chadema Maimuna Mpogole amewaomba wananchi wenye uwezo kujitoa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwani wao walichokitoa ndicho walichojaaliwa.

Aidha watoto waliofika kupata msaada huo Amina Chande na Amoni Swai wameshukuru kupata msaada huo kwa namna ya kipekee kutokana na hali ngumu walizokuwa nazo na kwa wakati tofauti wameomba wadau wengine kuendelea kutoa misaada hiyo kwa watoto wasiojiweza.




Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment