KAMATI ya mashindano ya Mei Mosi Taifa imesikitishwa
na kupungua kwa timu shiriki katika mashindano ambayo yamezinduliwa leo uwanja
wa Samora na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Juma Masenza.
Kauli hiyo imetolewa na makamu mwenyekiti wa kamati
ya michezo ya Mei Mosi Kitaifa Joyce Benjamini wakati wa uzinduzi wa michezo ya
Mei Mosi kwenye kiwanja cha kumbukumbu ya Samora Mkoani Iringa ambapo amesema
timu zimepungua kutoka timu kumi na Tano (15) mwaka jana hadi timu kumi (10)
mwaka huu wa 2018.
Benjamini alisema kuwa kupungua kwa idadi
ya timu shiriki kunatokana na baadhi ya mashirika ya sekta za UMMA na Serikali
kushindwa kupeleka timu kwa visingizio vya ukata ili hali timu ya Rais ikiwa
imeshiriki mashindaano hayo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunapenda kutoa malalamiko yetu juu ya
kupungua kwa hizi timu na kusingizia ukata wa pesa jambo ambalo sio kweli kwa
kuwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais wetu ni viongozi wapenda michezo hivyo
uoga wao ndio umefanya kushindwa kuzileta timu zao zishiriki mashindano haya”. Alisema
Benjamini
Benjamini alisema kuwa hakuna mahali ambako Rais
amekataza wafanyakazi wa Serikalini kutoshiriki michezo mbalimbali, viongozi
wetu wa serikali wamekuwa waoga kwenye matumizi ya fedha za Serikali, anachokitaka
Rais ni uhalisia wa matumizi ya fedha katika maeneo husika.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hata ukiangalia kwenye Ilani
ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 hadi mwaka 20102 ibara ya 61 ukurasa wa
218 hadi 219 unasema wajuu ya kuinua na kuendeleza michezo hapa nchini,sasa
kwanini Viongozi hawafuati Ilani hiyo”. Alisema
Benjamini.
Benjamini alizitaja timu zinazoshiriki mashindano
hayo Mkoani Iringa kuwa ni timu kutoka Ofisi ya Rais –Ikulu,Wizara ya Uchukuzi,
Chuo Kikuu kishiriki cha Afya na sayansi (MUHAS), Hifadhi za Ngorongoro, Geita
gold mine (GGM), Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA),Shirika la umeme Tanzania
(TANESCO), Tumbaku-TTPL ya Morogoro, Ukaguzi na Wenyeji timu ya RAS Iringa.
Naye Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza
aliyewakilishwa na Afisa Elimu Mkoa wa Iringa Majuto Njanga amezionya timu
ambazo zinashiriki kwenye Michuano ya Mei Mosi kuacha kuchukua wachezaji ambao
sio wafanyakazi kwani kufanya hivyo kunapunguza ladha ya mashindano
hayo.
Njanga amesema kuwa michezo hujenga undugu na furaha baina ya
wanamichezo hivyo kuwaingiza wachezaji ambao sio wafanyakazi kwenye mashindano
hayo wataondoa maana halisi ya mashindano hayo jambo ambalo linaweza kuwafanya
kushindwa kufikia malengo yao waliojiwekea.
“Mashindano haya ni ya wanamichezo wafanyakazi,kuna wale
wanamichezo ambao sio wafanyakazi ambao wanajulikana kama mamluki au wavamizi
kwamba hapa sio mahala pao nawasihi tuchezeshe wafanyakazi halisi ili mshindi
apatikane kihalali na sio vyenginevyo kwa sababu ni hatari sana kumleta
mwanamichezo ambaye sio mfanyakazi kwenye michezo hii anaweza kuvunjika mguu au
akifa kwa mfano hatuombei itokee hiyo itakuwaje “Alisema Njanga
Aidha Njanga alizitaka timu hizo kuacha kuwatumia
wachezaji wa aina hiyo kwani wana madhara makubwa hasa pale yanapokuwa
yakijitokeza kwa kuzitaka timu zenye utamaduni huo kuhakikisha wanaondokana
nao.
Akizungumzia waamuzi wanaochezesha mashindano hayo, Njanga aliwataka
kuchezesha kwa haki bila upendeleo kwa kufuata sheria za mchezo husika ili
mshindi aweze kupatikana kihalali kwa sababu wakienda kunyume chake wanaweza
kusababisha tafrani na manung’uniko kwa baadhi ya timu shiriki.
Hali kadhalika aliwataka kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya hali
ya juu wakati wote wa mashindano ikiwemo kukubaliana na matokeo pindi
watakapojikuta wamefungwa wakati wa mashindano hayo.
Baadae Njanga alikagua timu zilizokuwepo uwanjani wakati wa
uzinduzi wa michuano hiyo ambayo inatarajiwa kufikia kikomo Tarehe 29 Mwezi huu
na kwa washindi kupewa zawadi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.
John Pombe Magufuli siku ya Mei Mosi ambapo atakuwa Mgeni Rasmi.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA UZINDUZI HUO
MGENI RASMI AKIZUNGUMZA
0 Maoni:
Post a Comment