MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeelezwa kuwa puto lililowekwa tumboni mwa mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme, IPTL, Harbinder Sethi anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha, linaweza kupasuka muda wowote na kuhatarisha maisha yake.
Mbali ya Sethi, mshitakiwa mwingine ni mfanyabiashara James Rugemarila ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh bilioni 309.
Wakili wa Utetezi, Hajra Mungula amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa Aprili 11, mwaka huu mahakama iliamuru Sethi alipelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kupatiwa vipimo pekee.
Amedai kuwa mshitakiwa huyo, hajapatiwa matibabu wala majibu na kwamba kwa wiki mbili sasa, hali yake ni mbaya kwa kuwa puto lililopo tumboni mwake, linaweza kupasuka muda wowote.
Mungula ametoa madai hayo baada ya Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Swai amedai kuwa Sethi alionana na jopo la madaktari kwa ajili ya kupatiwa vipimo na kwamba wameeleza kuwa majibu yake atapatiwa Aprili 26, mwaka huu.
Hata hivyo, Hakimu Shaidi alisema kuwa ni jambo jema kuona kwamba mshitakiwa amepelekwa hospitali kama alivyoagiza.
Alisisitiza mshitakiwa huyo apatiwe matibabu. Pia aliutaka upande wa mashitaka kuhakikisha wanakamilisha upelelezi ili kesi hiyo iweze kuisha kwa haraka. Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 10, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
0 Maoni:
Post a Comment