RAIS John Magufuli ameshangazwa na hatua ya wafanyabiashara wadogo na wamachinga kufukuzwa na kupigwa faini kubwa kwa kutosajiliwa huku kampuni kubwa ya uchimbanji madini nchini Acacia ikiendesha shughuli zake bila kusajiliwa.
Akizungumza leo (Jumatatu) Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akipokea ripoti ya pili ya mchanga wa madini uliopo katika makontena 277 yaliyozuliwa bandarini amesema, ni jambo la ajabu kwa kampuni hiyo kufanya biashara ya matrilioni ikiwa haijasajiliwa kokote.
“Nimesoma katika ripoti hii, kampuni hii inafanya biashara kinyume cha sheria, haijasajiliwa mahali popote, hata brela haiitambui lakini inafanyabiashara ya matrilioni,” amesema Rais Magufuli.
Amesema ni lazima viongozi na wote waliopewa madaraka wajiulize ni mara ngapio wamekuwa wakiwafuata Watanzania wanaofanya biashara zao bila kusajiliwa kwa bunduki na kuwafukuza wamachinga ambao hawana leseni za biashara.
"Mwenyezi Mungu alituwekea rasilimali nyingi ili zitunufaishe Watanzania...madini tuliyonayo Watanzania ni madini ya kila aina na wala sio machache " ameongeza.
"Pamoja na mali hii yote, Mungu kutupendelea watanzania tumeendelea kuwa masikini, nina uhakika hata shetani aliko kule anatucheka kuwa umasikini wetu ni wa kujitakia, lakini shetani huyu huyu tunayemlani inawezekana aliwatumia baadhi ya Watanzania wakati wakiwa ni viongozi kutusababisha tuwe masikini," amesema.
0 Maoni:
Post a Comment