Lema kuendelea kukaa rumande

 

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha imeruhusu maombi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kukata rufaa ya kuomba dhamana yake ndani ya siku 10 kuanzia jana. Wakati mahakama hiyo ikiruhusu hilo, tayari mawakili wa Lema wamesajili rufaa namba 126/2016 katika mahakama hiyo jana jioni.
Awali akizungumza kuhusu ruhusa hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Dk Modesta Opiyo alisema hakukuwa na ucheleweshwaji wowote wala ukiukwaji wa sheria kwa mawakili wa Lema, walioufanya wakati wa uwasilishaji wa maombi ya kuongezewa muda wa kukata rufaa.
Akisoma uamuzi wa kama maombi hayo ya Lema yalikuwa ndani ya muda au la, Jaji Opiyo alisema maombi hayo yalikuwa ndani ya muda kwa sababu mawakili wa serikali walihesabu siku hadi za mwisho wa wiki (Jumamosi na Jumapili).
Alisema hakukuwa na uvunjaji wa sheria, uliofanywa na mawakili wa mbunge huyo, bali mawakili wa serikali wao waliweka pingamizi zao wakahesabu hadi siku za mapumziko.
"Mahakama hii imemruhusu Lema kukata rufaa ndani ya siku kumi kuanzia leo hii, pia busara ya mahakama ni lazima iangaliwe katika kuamua jambo hili la uamuzi wa rufaa hii, hivyo mawakili wa Lema hawakuwa nje ya muda kama ilivyodaiwa na mawakili wa serikali," alisema.
Akichambua hoja za mabishano ya kama nia ya notisi ya kukata rufaa ilipitiliza muda wake au la Jaji Opiyo, alisema awali alitupilia mbali pingamizi wiki iliyopita baada ya kupitia hoja za pande zote.
Alisema kuwa pingamizi hizo za serikali, walizokuwa wakitaka maombi hayo yasisikilizwe kuwa mawakili hao hawakuwa na hoja za kisheria zenye mashiko.
Maombi hayo namba 69, upande wa serikali ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na wakili, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.
Akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga alidai mahakamani hapo kuwa maombi hayo, yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya Kifungu 361(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alidai kuwa maamuzi wanayotarajia kukatia rufaa ni uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia maamuzi hayo rufaa kuwa ni kuiomba mahakama hiyo, ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na mahakama ya chini.
Alisema kuwa uamuzi huo, ulimpa mleta maombi (Lema) dhamana, ila kabla hajapewa masharti ya dhamana, upande wa Jamhuri ulitoa notisi ya nia ya kukata rufaa. Alidai mahakamani hapo kuwa wanaiomba mahakama hiyo, iwape muda ambao hautazidi saa 1:30 kwa ajili ya kuleta notisi hiyo ili mahakama iweze kurekebisha makosa hayo, yaliyofanyika na mahakama ya chini.
Akiwasilisha hoja ya pili, Wakili Mangula alidai mahakamani hapo kuwa tangu kutolewa kwa uamuzi huo, hawakuwa wamepumzika, muda wote walikuwa mahakamani na walikuwa wanakuja kwa njia tofauti ili kuiomba mahakama irekebishe makosa hayo ya kisheria.
Alisema baada ya uamuzi huo kutolewa, muda wa kazi ulishaisha na ilikuwa siku ya ijumaa, hivyo Novemba 14 mwaka huu walipeleka barua ya malalamiko mahakamani hapo. Walipoitwa pande zote mbili katika shauri namba 6, walikumbana na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa serikali.
Akijibu hoja za waleta maombi hao, Wakili Ngole alidai kuwa ni wazembe na kuwa hata uamuzi wanaolalamikia mahakamani hapo.
Awali ulimpa mleta maombi dhamana, lakini kabla hajapewa masharti ya dhamana, mahakama iliingiliwa mamlaka yake na hawajawasilisha maombi hayo.
Wakili huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na makosa yoyote ya kisheria, kama inavyodaiwa na waleta maombi hao na kudai kuwa baada ya hakimu kusema mahakama inampa mshitakiwa dhamana, Jamhuri kwa haki yake, walisimama na kuifahamisha mahakama wana nia ya kukata rufaa.
Baada ya Jaji Opiyo kutoa uamuzi huo, mawakili wa Lema wakiongozwa na Mfinanga pamoja James Millya, waliweza kuwasilisha mahakamani nia yao ya kukata rufaa na ilipokelewa mahakamani hapo. Inasubiri tarehe ya kupangiwa Jaji pamoja kusikiliza kwa dharura na hatimaye Jaji huyo atakayepangiwa, kuamua kama apate dhamana au la.
Nje ya mahakama, watu mbalimbali waliohudhuria kesi hiyo walikuwa na furaha huku wakikumbatiana, wakiwemo ndugu wa Mbunge huyo. Lema alirudishwa mahabusu iliyopo Gereza la Kisongo kwa ajili ya kusubiri kuwa nje kwa dhamana au la.
Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma, ambapo alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu akikabiliwa na mashitaka ya uchochezi ikiwemo kumtukana Rais John Magufuli. Mawakili wa Lema walidai kuwa tayari jana jioni wamesajili rufaa hiyo namba 126 ya mwaka 2016.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment