Mwanamke
aliyekuwa akiamini kuwa mtoto wake angefufuka siku ya tatu baada ya
kufariki dunia Februari 15, jana alizua kizaazaa baada ya kufukua kaburi
na kutoa maiti hiyo, hali iliyosababisha wananchi wafanye vurugu na
kuichoma nyumba yake.
Mtoto
huyo, Baraka Mwafongo (22), aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu,
alizikwa siku iliyofuata lakini maiti yake ilifukuliwa usiku wa kuamkia
jana na kuwekwa katika pagala ikiwa imevishwa suti kumsubiri mchungaji
aifufue.
Mwanamke
huyo, Ruth Segeleti (52), anayeishi Mtaa wa Shigamba, Mbalizi, hakutaka
kuzika maiti ya mwanawe akieleza kuwa mtoto wake angefufuka baada ya
siku tatu, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri
Kidavashari.
Alisema
polisi waliona kuwa huenda hana uwezo ndipo walipomsaidia kuzika,
lakini usiku wa kuamkia jana alipata vijana wawili waliomsaidia kufukua
kaburi na kuchukua maiti hiyo ambayo waliipeleka kwenye pagala na
kuiweka ikiwa imevishwa suti.
Baada
ya wakazi kubaini kaburi la mtoto huyo limefukuliwa, kundi la watu
lilijitokeza makaburini na kusababisha polisi kufyatua mabonu ya
machozi
Wananchi
waligundua kuwa kaburi lilikuwa wazi majira ya saa 3:00 asubuhi baada
ya majirani kumuona mwanamke ambaye walijua alikuwa na msiba wa mtoto
wake Jumamosi akiwa na jembe mkononi na furushi la nguo akitokea
makaburini.
“Nilipomsemesha, hakutaka kunijibu,” alisema mkazi wa mtaa huo, Mariam Mwakisepile ambaye ni jirani wa mwanamke huyo.
“Nililazimika kuwaarifu majirani wengine ambao walikwenda makaburini ambako walikuta kaburi la Baraka likiwa limefukuliwa.”
Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Christina Nyopelo alisema walipiga simu kituo cha polisi cha Mbalizi na kuwaarifu.
“Baada ya muda mfupi polisi waliwasili na wakiwa makaburini waliona sanduku ndani ya kaburi, lakini mwili haukuwapo,” alisema Nyopelo.
“Polisi
kwa kushirikiana na wananchi waliamua kukagua maeneo ya makaburi na
hatimaye walifanikiwa kuukuta mwili ukiwa umelazwa kwenye banda lililopo
karibu na eneo hilo.”
Habari hizo zilisambaa na kukusanya kundi la watu kutoka mji wa Mbalizi na kusababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Alisema
baadaye polisi walikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo na kumkamata, pia
waliupeleka mwili wa Baraka, Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya
kuuhifadhi.
Kamanda Kidavashari alisema mtuhumiwa alipelekwa Kituo cha Polisi Mbalizi kuhojiwa.
Umati wa watu pia ulijazana Mtaa wa Shigamba na kusababisha polisi walipue mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu.
Jitihada
hizo zilizaa matunda kwa muda mfupi, lakini ilipofika saa 8:00 mchana
watu wasiofahamika waliichoma moto nyumba ya mwanamke huyo.
Katika
kukabiliana na tukio hilo, polisi waliwatawanya wananchi kwa kupiga
baadhi ya watu waliokutwa eneo la tukio. Kamanda Kidavashari alisema
polisi wanawasaka watu waliohusika kuchoma moto nyumba ya mwanamke huyo.
0 Maoni:
Post a Comment