Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Simon Siro amesema endapo Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe hataripoti kituoni kesho (saa 48 tangu jana), atatafutwa
kwa namna ambayo jeshi hilo litaona inafaa.
Mbowe ni miongoni mwa watu
mashuhuri waliotajwa hivi karibuni katika orodha ya watu 65 ya Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wanaodaiwa kujua taarifa za
wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamishna Siro alisema Mbowe kupitia kwa baadhi ya viongozi
aliwajulisha angeripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Jumatano
ya Februari 15, lakini alikuwa hajaripoti hadi jana
“Jumatatu
asiporipoti kutakuwa hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi
kutafuta namna ya kumuhoji,” alisema.
“Mheshimiwa Mbowe tunamheshimu
sana kama kiongozi wa chama kikubwa cha siasa na hata akiwa bungeni
ameonekana akipinga kwa nguvu suala la dawa za kulevya na anasikitika
kuona vijana wa Kitanzania wanateketea.
"Asitafute namna nyingine,
tunamuhitaji kwa ajili ya kumuhoji kutokana na hizi tuhuma za dawa za
kulevya,” alisema Siro.
Alisema kiongozi kama Mbowe hatakiwi kuwa mtu wa
kuta- futwa. ”Jeshi la Polisi lisingependa kuwa na mvutano na yeye,
najua anajua kuwa tunamtafuta.
"Jana (juzi) tumejitahidi kumtafuta kwa
simu hajapatikana, tumekwenda nyumbani kwake hatujampata na hata
tulipokwenda mahali ambapo inasemekana anaishi sasa hatukumpata,”
alisema.
Kamanda Siro alisema hafahamu ni kwanini Mbowe haja- ripoti
wakati yeye mwenyewe anapinga biashara ya dawa za kulevya, hivyo baada
ya taarifa yake ya jana, anamuomba ajitahidi aende waonane, tofauti na
hapo ni lazima atakamatwa na kuhojiwa kwa kuwa ndiyo wajibu wa jeshi
hilo.
Hata hivyo, Februari 10 akiwa mjini Dodoma, Mbowe alise- ma
hatafika polisi kwa kuitwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda lakini yupo tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola endapo
utaratibu wa kisheria utafuatwa.
Wengine kortini
Katika hatua nyingine, Kamishna Siro
alisema operesheni ya dawa za kulevya inaendelea vizuri na kesho
watuhumiwa Agnes Gerald ‘Masogange’, Rashid Said ‘Chid Mapenzi’ na Walid
Nasher watapelekwa mahakamani.
Hata hivyo, Kamanda Siro alitoa kauli
mbili zinazokinzana, mwanzo alisema watuhumiwa hao watashtakiwa kwa
kutumia dawa za kulevya, lakini baadaye akasema walipatikana na dawa
hizo.
Alisema operesheni inayoendelea tangu Februari 16 imewezesha
kukamatwa watuhumiwa 73 wa makosa mbalimbali, yakiwamo ya wizi wa
kutumia nguvu.
Pia, ilikamatwa mitambo mitano ya kutengeneza pombe
haramu aina ya gongo na puli 250 za bangi. Kamishna Siro alisema juzi
walimkamata mtuhumiwa anayejifanya askari magereza akiwa na sare za
jeshi hilo.
Alisema mtuhumiwa huyo, Elias Msingwa aliwahi kuwa askari wa
jeshi hilo kabla ya kuachishwa kazi Desemba mwaka jana, akiwa na cheo
cha Koplo lakini amekamatwa akiwa na sare zikiwa na cheo cha Sajenti.
Akizungumzia tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam,
akiwa na pingu mkononi, Msingwa alisema alikuwa askari katika Gereza la
Keko jijini Dar es Salaam na alifanya kitendo hicho baada ya kukosa nauli ya
daladala.
“Ninakaa Kivule jana (juzi) nilikuwa sina nauli ya kuja mjini
ndiyo maana nikavaa sare hizi ili niweze kusafiri bure, ninaomba radhi
kwa Watanzania na kuwashauri wenzangu wasije wakafanya hivi na baada ya
hapa nitazirudisha sare hizi,” alisema Msingwa.
Kamishna Siro alisema
sare hizo zilivaliwa kinyume na sheria, huku zikitumika kuwababaisha
wananchi hivyo upelelezi unaendelea utakapokamilika jalada lake
litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
0 Maoni:
Post a Comment