Picha ya tukio sio husika
SIKU chache kabla ya jamii nchini haijasahau tukio la Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mbeya la kumdhalilisha Mwanafunzi,tukio hilo limejirudia katika shule ya Sekondari ya Ihanga Jijini Mbeya baada ya mwanafunzi wa Kidato cha pili jinsi ya kiume kuchaniwa suruali kisha kutembezwa utupu madarasa yote huku akizomewa na wanafunzi.
Akisimulia tukio hilo mzazi wa mwanafunzi huyo Joseph Bisale Sanga mkazi wa Soweto jijijni Mbeya amesema tukio hilo limetokea mwishoni mwa juma baada ya kijana wake kuvaa suruali isiyotakiwa siku hiyo ndipo Mwalimu Mapunda alimwadhibu kwa kumchapa viboko tisa.
Hata hivyo Mwalimu Bathromeo Kibona alimchania suruali hiyo ikidaiwa haiko katika sare za shule hivyo alivua viatu vya mwanafunzi na kuichana ambapo sehemu ya viungo ilikuwa ikionekana huku akitembezwa madarasa yote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na wanafunzi wa jinsia zote wakishuhudia udhalilishaji huo.
Mkuu wa Shule hiyo Theresia Mwaifwani amekiri kutokea kwa tukio hilo lakini amesema Mratibu wa Elimu Kata ndiye mwenye jukumu la kulizungumzia ambapo Mratibu wa Elimu Mwalimu Magdeni Sindika amekiri kutokea tukio hilo na kwamba mwanafunzi Kalebu Mwita alikiuka kanuni za shule.
Aidha Sindika amesema adhabu iliyotolewa na walimu hao ni kubwa kwa mujibu wa sheria na kwamba watajadiliana na Afisa Elimu Jiji ili kuona adhabu wanayostahili walimu hao pia alimuomba Mzazi awasamehe walimu hao kwa kosa walilolifanya na kuadidi kumtafutia shule mwanafunzi huyo ili asome bila fedheha.
Kwa upande wake Mzazi wa mwanafunzi huyo Joseph Mwita amesema hapingi adhabu iliyotolewa na walimu lakini anapinga kitendo cha kuchaniwa suruali na kudhalilishwa kwa wanafunzi wenzie hali inayomfanya kijana wake kuathirika kisaikolojia.
Naye mwanafunzi Kalebu Mwita amesema kuwa suruali aliyovaa ni ya shule isipokuwa siku hiyo alivaa suruali nyeusi badala ya kahawia si kwamba alivaa suruali ya kubana kama inavyodaiwa na walimu na pia adhabu ya viboko ilitosha lakini kitendo cha kuchaniwa suruali na kutembezwa madarasa yote kimemsononesha sana.
Kwa upande wake Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mbeya Protas Mpogole amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba Halmashauri ya Jiji kitengo cha elimu kinalishughulika suala hilo.
0 Maoni:
Post a Comment