SERIKALI imesema haijawekeza kwa kiwango kikubwa katika afya ya
mwanamume upande wa afya ya uzazi, lakini zipo tafiti mbalimbali
zikiwemo za nje ya nchi, ambazo zimekuwa zikionesha kuwepo kwa hali ya
kushuka kwa nguvu za kiume.
Hata hivyo, imesema ipo dawa ijulikanayo kama ‘Ujana’ ambayo
imesajiliwa na Baraza la Usajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, ambayo
inalenga katika kuongeza nguvu za kiume. Imesema upo utafiti kuhusu afya
ya wanaume, unaofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMRI), ambao umefikia katika hatua nzuri, ambayo ni katika
ufungashaji. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Faustine Ndugulile alisema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumzia usajili wa dawa za tiba asili na tiba mbadala.
Ndugulile alisema Tanzania haijafanya utafiti kuhusu eneo hilo la
afya ya uzazi kwa wanaume, kama ilivyo kwa hali ya uzazi kwa wanawake na
watoto nchini, lakini ili kujua tatizo lipo kwa kiwango gani licha ya
kwamba takwimu za kidunia zinazoonesha eneo hilo kuwa tatizo. Alitaja
sababu zinazochangia kupungua kwa nguvu za kiume kuwa ni kutofanya
mazoezi, ulaji wa vyakula visivyo bora kiafya na kula vyakula vyenye
mafuta kwa wingi. Nyingine ni utumiaji wa vilevi ikiwemo pombe na sigara
na ulaji wa nyama za mifugo inayofugwa,huku ikikuzwa kwa kuwekewa dawa
ikiwemo kuku, ambavyo kwa pamoja huathiri mnyororo mzima. Alisema ipo
haja kwa serikali kuangalia na kuona iwapo utafiti ufanyike ili kubaini
hali ikoje nchini.
Kuhusu dawa ya Ujana alisema ni mojawapo ya dawa tano, zilizosajiliwa
na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Aliwataka waganga wa tiba
asili na tiba mbadala, kutotangaza dawa za asili katika vyombo
mbalimbali vya habari iwapo hazijasajiliwa. “Serikali inatambua tiba
asili na mbadala lakini kumekuwepo na wimbi kubwa la waganga kutangaza
dawa zao kinyume na utaratibu wa sheria huku wakijua kuwa mamlaka pekee
ya usajili ni baraza ndio wenye kutoa ruhusa ya kitu gani kitangazwe,”
alisema.
Aliongeza kuwa ni marufuku waganga kutoa matangazo bila kuwa na
kibali kutoka baraza na kwamba matangazo yao, yanatakiwa kutambulisha
wako wapi, mawasiliano na si dawa hiyo ina uwezo wa kutibu ugonjwa gani.
Hata hivyo, Ndugulile alisema kumezuka wimbi la kuingizwa nchini
mashine zikidai zina uwezo wa kutoa sumu na kupima magonjwa yote kwa
wagonjwa, ambapo zinakuwa hazijapimwa na wala kutokuwa na vibali ikiwemo
mashine ijulikanayo kama ‘Kwanta’.
Alitoa agizo kwa Msajili wa Tiba
Asili na Mbadala, kusaka mashine hizo na kuzikamata, ambapo msako
ulifanyika kwa siku mbili Machi 6 na 7 mwaka huu. Akitaja dawa ambazo
tayari zimesajiliwa na baraza hilo, Msajili Dk Ruth Suza alisema ni IH
Myoon, Ujana, Coloidal Silver, Sudhi na Vatari.
0 Maoni:
Post a Comment