TUME ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) imetangaza uchaguzi wa marudio wa urais kufanyika Oktoba 17 mwaka huu.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati alisema jana kuwa uchaguzi huo utashirikisha wagombea wawili pekee wa urais, Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga.
“Hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wa urais katika uchaguzi huo upya. Waliopinga matokeo ya uchaguzi kortini ni Raila Odinga na mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza, William Ruto, watakuwa ndio wagombea pekee,” taarifa ya Chebukati ilisema.
Awali, akizungumza na gazeti hili jana, Balozi wa Kenya nchini, Boniface Muhia alisema kwamba uchaguzi huo, lazima ufanyike ndani ya siku 60 kama Mahakama ilivyoamuru na hivyo wanasubiri taarifa kamili kutoka Tume ya Uchaguzi.
Muhia alisema Tume hiyo ilitarajiwa kukutana kati ya jana na leo, kujadili mambo mbalimbali kuhusu uchaguzi, ikiwemo kupanga tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Alisema kila upande (Jubilee na Upinzani) wako tayari kushiriki uchaguzi huo wa marudio.
Ikumbukwe kwamba, katika Uchaguzi Mkuu ulifanyika Agosti 8 mwaka huu, IEBC ilimtangaza Rais Uhuru Kenyatta kutoka chama tawala cha Jubilee kuwa mshindi wa urais kwa kupata kura milioni 8.2 sawa na asilimia 54.27, wakati mgombea wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga alipata kura 6.7 sawa na asilimia 44.74.
Ushindi huo wa Rais Kenyatta ulipingwa mahakamani na Mgombea wa Nasa, Raila Odinga. Ijumaa iliyopita Mahakama ya Juu nchini Kenya, ilitoa maamuzi ya kesi hiyo kwa kuamuru uchaguzi wa urais urudiwe ndani ya siku 60 baada ya kubaini kuwa kulikuwa na dosari kwenye uchaguzi uliopita.
Jopo la majaji sita wakiongozwa na Jaji Mkuu, David Maraga walisikiliza kesi hiyo na miongoni mwao, majaji wanne walikubaliana uchaguzi urudiwe na wengine wawili hawakukubaliana na maamuzi hayo ya majaji wenzao.
Baada ya maamuzi hayo ya Mahakama, Rais Kenyatta alisema anaheshimu maamuzi ya mahakama ingawa hakubaliani nayo; na alitoa wito kwa Wakenya kudumisha amani. Odinga aliishukuru mahakama kwa maamuzi hayo na kusema kwamba mahakama nchini humo sasa imejitambua.
0 Maoni:
Post a Comment