Mawakili
kutoka nje ya nchi wanaomtetea bilionea wa kampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi, kuhusu
kupewa dhamana, jana walikwamisha usikilizwaji wa maombi hayo.
Bilionea
huyo na mwenzake James Rugemalira, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu
uchumi wakidaiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya
Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), isivyo halali.
Pia,
wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo ni miongoni mwa
mashtaka yasiyo na dhamana, lakini washtakiwa, kila mmoja kwa wakati
wake wameamua kusaka dhamana katika Divisheni ya Makosa ya Uhujumu
Uchumi na Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka amemuwekea pingamizi bilionea huyo katika
maombi yake hayo, ambalo lilipangwa kusikilizwa jana na Jaji Winfrida
Korosso, lakini usikilizwaji wa pingamizi hilo ulikwama baada ya
bilionea huyo kuamua kuyaondoa mahakamani maombi hayo.
Seth
aliamau kuyaondoa mahakamani maombi hayo kutokana na kuhusisha mawakili
kutoka nchini Afrika Kusini, ambao aliwakodi kuongeza nguvu kwa
kushirikiana na mawakili wazawa kumpigania katika dhamana yake hiyo.
Maombi
ya kuyaondoa maombi hayo mahakamani yalitolewa na kiongozi wa jopo la
mawakili wanaomtetea bilionea huyo, Melkizedeck Lutema, baada ya
kubainika mawakili hao wa nje hawakuwa na sifa za kufanya kazi nchini.
Ingawa
mawakili hao walikuwa hawajatambulishwa mahakamani, lakini katika
nyaraka mbalimbali zinazohusiana na maombi hayo, wametajwa kuwa miongoni
mwa mawakili wake.
Kutokana
na kasoro hiyo Wakili Lutema aliiomba mahakama iyaondoe maombi hayo kwa
lengo la kuanza upya mchakato wa kuyawasilisha mombi ambalo mahakama
iliridhia.
Wakili
wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango, alisema mawakili hao hawana cheti
cha kufanya kazi katika mahakama za hapa nchini kutoka kwa Jaji Mkuu.
Wakili
Mango alisema kuwa ili wakili kutoka nje ya nchi aruhusiwe kufanya kazi
katika mahakama za ndani ni lazima aombe kibali kutoka kwa Jaji Mkuu
ambacho analazimika pia kukilipia, jambo ambalo mawakili hao hawakuwa
wamelifanya.
Seth
na Rugemalira wanakabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye jumla
ya mashtaka 12 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa mujibu wa
sheria za Tanzania mashtaka hayo hayana dhamana na hadi sasa washtakiwa
wanasota mahabusu.
0 Maoni:
Post a Comment