MBUNGE MHE ZUENA BUSHIRI AMEWATAKA MAAFISA WATENDAJI KUTOKA MAOFISINI KWENDA KWA WANANCHI

 

VIJANA Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia kumi ambayo imekuwa ikitolewa na Halmashauri mbalimbali nchini kwaajili ya kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo hiyo isiyokuwa na riba.

Wito huo umetolewa leo Aprili 14, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa viti Maalumu Mkoani Kilimanjaro Mheshimiwa Zuena Bushiri wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.

Mbunge huyo amesema kuwa mnamo mwezi Februari 2026, Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 200 kwaajili ya mikopo ya vijana ikiwa ni jitihada za Rais Samia katika kuwakwamua vijana kiuchumi waweze kufanya biashara zao na kusaidia familia zao.

Ameishauri Serikali kupitia mikopo hiyo kusimamia vizuri utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo ili ikatumike kwa lengo lililokusudiwa ili vijana waweze kunufaika ipasavyo.

Katika mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri nchini, Mbunge Zuena amesema zipo baadhi ya changamoto ikiwemo ujazaji wa dodoso, akisema wapo baadhi ya watu wamekuwa wakishindwa kujaza madodoso hayo wakiwemo wananchi wa vijijini.

Amesema asilimia kubwa ya mikopo hiyo ambayo imekuwa ikiwalenga akina mama wa vijijini ambao hawawezi kufanya biashara kubwa, maafisa maendeleo ya jamii wamekuwa wakiwatuma na kuwaambia wakajaze dodoso jambo ambalo hawawezi na matokeo yake wamekuwa wakienda kwenye huduma za Stationery ambako hutozwa fedha.

Ameishauri Serikali kusimamia vizuri swala hilo kwa kuwatoa maafisa maendeleo ya jamii na kata maofisini na kushuka chini kwa wananchi kwa makundi yote ili wawasaidie waweze kupata fedha hizo za mikopo iwasaidie kwenye biashara zao.

Awali akichangia Hotuba ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Zuena aliipongeza Serikali kwa kuwajali wananchi wake kwa kupiga hatua kubwa kwenye maswala ya Afya kuanzia ngazi ya Kata hadi kanda.

Amewataka wananchi kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya Afya nchini akisema hotuba hiyo inaonyesha kuwa mwaka 2024 Taifa lilikuwa na vituo vya kutolewa huduma za afya kwa asilimia 80 na kwamba hadi mwezi Februari 2026 wastani wa utoaji huduma ni asimilia 89 akisema ni hatua kubwa imepigwa na Serikali.

Amempongeza Rais Samia kwa kuhakikisha huduma za kibingwa na bobezi zinapatikana nchini ikiwa awali wananchi wengi walilazimika kusafiri kwenda nchi za nje hasa India kwaajili ya kutafuta matibabu na vipimo ambavyo kwasasa vinapatikana nchini akitolea mfano wa kipimo cha Ugonjwa wa Saratani na huduma ya upandikizaji wa figo ambayo inapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili na Benjamin Mkapa Dar Es Salaam.

Ameishauri Serikali kuongeza ajira ya watumishi kwenye kada ya afya ili iendane na idadi ya vituo vya kutolea huduma sanjari na kuiomba Serikali kushusha huduma ya tiba mtandao kuanzia Hospitali za Rufaa hadi za Wilaya.


Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment