Pacha
walioungana ambao walikuwa wakitumia pamoja baadhi ya viungo vya ndani,
wamefariki dunia juzi jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa
na umri wa siku 26.
Daktari
bingwa wa upasuaji wa watoto wa hospitali hiyo, Zaituni Bokhari alisema
jana kuwa watoto hao wamefariki dunia baada ya kupata maambukizi ya
kifua kwa muda mfupi.
Alisema
kutokana na hali waliyokuwa nayo ilikuwa ni rahisi kwao kupata
maambukizi mbalimbali hasa kwenye mapafu na katika baadhi ya viungo
vyao.
“Walikuwa
wanaendelea vizuri sana ila (juzi) jana ndiyo walibadilika ghafla,
wakaanza kuonekana wanapata tatizo la kupumua, hata hivyo, mmoja
alizaliwa na tatizo la kupumua,” alisema Dk Bokhari.
Watoto hao walizaliwa katika Hospitali ya Misheni ya Berega, Morogoro, Julai 21.
Kutokana
na hali zao, Julai 24 walifikishwa Muhimbili ambako walichukuliwa
vipimo mbalimbali vya kuchunguza afya zao na kuangalia uwezekano wa
kuwatenganisha.
Baada
ya kufanyiwa vipimo vya kimaabara kwa takribani wiki nzima,
iligundulika kuwa wanatumia pamoja baadhi ya viungo vya ndani ikiwamo
moyo na ini.
Majibu hayo yalikuja baada ya vipimo vya radiolojia vikiwamo CT Scan, MRI, X Ray, moyo (ECO) pamoja na vipimo vyote vya damu.
Mbali
ya kugundulika kuwa wanatumia pamoja baadhi ya viungo vya ndani ikiwamo
moyo na ini, Dk Bokhari alisema watoto hao wameungana sehemu ya kifua
na tumbo na baada ya vipimo vya CT Scan, ikaonekana pia kwamba kuna
baadhi ya ogani zimeshikana.
Pia
alisema majibu hayo ya CT Scan ya tumbo na kifua yalionyesha kuwa kuna
chemba nyingi za milango ambazo walikuwa wakishirikiana.
Pamoja
na hali hiyo, Dk Bokhari alisema jopo la madaktari lilikuwa limejiandaa
kuwatenganisha watoto hao na kwamba kazi hiyo ilikuwa ifanyike katika
miezi sita ijayo.
0 Maoni:
Post a Comment