HATIMAYE Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ameachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kulala mahabusu ya gereza la Segerea kwa siku tatu.
Licha ya kulala gereza la Segerea tangu Julai 20, mwaka huu alipokamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Lissu alikuwa mikononi mwa Polisi na kwamba jana aliachiwa kwa kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh milioni 10.Hatua hiyo imetokana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kutupilia mbali ombi la upande wa mashitaka, ulioomba mahakama kumnyima dhamana Lissu kwa sababu ya usalama wake.
Upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na mawakili, Fatuma Karume na Peter Kibatala, uliomba mshitakiwa huyo apewe dhamana. Akitoa uamuzi dhidi ya maombi hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alisema upande wa mashitaka, ulishindwa kutaja kesi ambayo Lissu aliwahi kuruka dhamana.
Pia alisema suala la usalama wa mshitakiwa, sio sababu pekee ya kumfanya anyimwe dhamana na kumuweka ndani. “Lissu ana kundi la Mawakili 18 ambao wamejitokeza kumuwakilisha hii inaonesha watu wanaupendo dhidi yake na hivyo wakasimama kidete kumtetea.
Hivyo mshitakiwa atakuwa nje kwa dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mdhamini asaini bondi ya Sh 10 milioni,” alisema Hakimu Mashauri. Pia alimtaka Lissu kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Baada ya kutolewa kwa masharti hayo, kesi iliahirishwa kwa muda wa nusu saa kusubiri wadhamini ambao walifika. Lakini, kutokana na ulinzi ulioimarishwa mahakamani hapo, Polisi waliwazuia kuingia mahakamani hapo.
Hata hivyo saa 3:34 asubuhi wadhamini waliingia mahakamani na kuwasilisha nyaraka zao, ambazo ndipo Lissu aliachiwa huru na kuondoka mahakamani hapo. Aidha, Wakili wa Serikali, Simon Wankyo alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali. Jopo la Mawakili wanne wa Serikali ambao ni Mutalemwa Kishenyi, Simon Wankyo, Paul Kadushi na Tulumanywa Majigo, waliwasilisha hoja mahakamani hapo wakiomba Lissu anyimwe dhamana kwa kuwa anakabiliwa na kesi zaidi ya nne za kutoa maneno ya uchochezi na izingatie usalama wake kwa kuwa anapandikiza chuki baina ya serikali na wananchi.
Aidha, jopo la mawakili 18 wanaomtetea Lissu, likiongozwa na mawakili Karume na Kibatala waliomba mteja wao apewe dhamana. Lissu anadaiwa kuwa Julai 17, mwaka huu maeneo ya Ufipa Kinondoni Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi ambayo ni ‘’Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini, vibali vya kazi (working permit) vinatolewa kwa wamishenari wa kikatoliki tu huku madhehebu mengine yakielezwa kupanga foleni uhamiaji.
“Viongozi wakuu wa Serikali wanachaguliwa kutoka kwenye familia, kabila na ukanda. Acheni woga pazeni sauti kila mmoja wetu . Tukawaambie wanaompa msaada wa pesa Magufuli na Serikali yake, kama tulivyowaambia wakati wa serikali ya makaburu, hii serikali isusiwe na jumuiya ya kimataifa, isusiwe na jumuiya ya kimataifa, isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi, yeye ni dikteta uchwara,” maneno ambayo yanaleta chuki
0 Maoni:
Post a Comment