Ngome ya Maalim Seif yabomoka

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua Wabunge wanane wa viti maalum wa Chama Cha Wananchi (CUF), baada ya waliokuwa wabunge kwenye nafasi hizo, kufukuzwa uanachama wa chama hicho na Spika kuridhia.

Julai 24, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba alitangaza kuwafukuza ubunge wabunge hao wanane kwa makosa mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu na kukihujumu chama huku moja ya mambo yaliyotajwa ni ile ya kumuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad (pichani) kwa kumuunga mkono kupambana na uongozi kwa kumsaidia kufungulia ofisi maeneo ya Magomeni jijini Dar es Salaam kinyume na utaratibu.

Pia alitaja kuwa sababu nyingine ni ya kukihujumu chama hicho, kwa maelezo kuwa walitaka kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumwondoa yeye (Lipumba) madarakani.

Juzi, Ofisi ya Spika wa bunge, ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema imepokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Taifa ya CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ikimuarifu kuhusu uamuzi wa Baraza Kuu la Chama hicho kuwafukuza wabunge wanane na madiwani wawili uanachama wa chama hicho kwa makosa kadhaa ya kinidhamu.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Kailima Ramadhani alisema jana (juzi ) usiku walipokea barua kutoka kwa Spika, kuwataarifu uwepo na nafasi za wabunge hao .

“Jana (juzi), usiku tulipokea barua kutoka kwa Spika ikitutaarifu uwepo wa nafasi hizo na kututaka kutekeleza kwa kujaza nafasi hizo, na sisi tuliwaandikia chama husika asubuhi na wakajibu na sisi tukateua na kuwasilisha kwa Spika majina,” alisema Ramadhan.

Aliwataja wateule hao kuwa ni Rukia Ahmed Kassim, Shamsha Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainabu Mndolwa Amir, Hindu Hamis Mwenda, Sonia Jumaa Magogo, Alfredina Apolinary Kahigi na Nuru Awadh Bafadhili.
Alisema majina yao tayari yameshawasilishwa kwa Spika, kwa hatua nyingine na pia chama kimeshapewa nakala ya uteuzi huo. Kailima alifafanua kuwa uteuzi huo ni kwa mujibu wa Ibara ya 78 kifungu kidogo cha nne cha Katiba pamoja na kifungu kidogo cha 86, A(8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura Namba 343.

“Tulipopata barua ya Spika, tulifanya kikao na wajumbe wa tume leo (jana) na tuliwateua wabunge hao baada ya kuwasiliana pia na chama husika na tayari tumeshapeleka majina kwa Spika,” alisema Kailima.
Aliongeza kuwa utekelezaji huo, umefanywa pia kwa mujibu wa Kifungu namba 37 kifungo kidogo cha (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa upande wake, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Jafar Mneke alisema wameshapata nakala ya majina ya wateule hao kutoka NEC.

“Baada ya Bunge kuridhia uamuzi wa chama wa kuwafukuza wabunge wa viti maalumu wanane na madiwani wawili, NEC wametutaarifu kwa barua juu ya hilo na sisi tumeshatekeleza wajibu wetu wa kupeleka majina manane, na wao wameshatekeleza na kuteua na nakala wametupa,” alisema Mneke.

Alisema kwa upande wa madiwani hao wawili, tayari chama kimeshaandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri za Manispaa za Ubungo na Temeke jijini Dar es Salaam, kuwataarifu uwepo wa nafasi hizo na wanachosubiri ni majibu ya barua hizo.

“Pia kwa nafasi za madiwani, tumeshawaandikia wenyeviti husika barua kuwajulisha uwepo wa nafasi za madiwani tunachosubiri ni majibu yao na ndipo hatua nyingine zifuate,” alisema Mneke.

Aidha, aliwatahadharisha wanachama wa chama hicho kuwa bado mchakato wa kuwafukuza wasaliti ndani ya chama, unaendelea na iwapo wabunge hata wa majimbo watabainika kuhusika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Wakizungumzia kuvuliwa kwao uanachama, Kiongozi wa wabunge wa CUF Bungeni ambaye naye amevuliwa uanachama, Riziki Ngwali alisema hadi sasa hawajapokea barua rasmi ya kuvuliwa uanachama wao.

Alisisitiza kwamba walichaguliwa kwa barua na lazima watenguliwe kwa barua. “Hatujapokea barua hadi sasa, lakini pamoja na hilo, sisi hatukubali uamuzi huo kwa sababu haujatolewa na mamlaka sahihi, tumeamua kwenda mahakamani kutafuta haki yetu,” alisema Ngwali.

Julai 25, mwaka huu Ofisi ya Spika wa Bunge, ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema imepokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Taifa ya CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ikimuarifu kuhusu uamuzi wa Baraza Kuu la Chama hicho, kuwafukuza wabunge wanane na madiwani wawili uanachama wa chama hicho kwa makosa kadhaa ya kinidhamu.

Wabunge waliofukuzwa uanachama na kuvuliwa ubunge wa viti maalumu ni pamoja na Serevini Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Alli Mohamed.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment