Viongozi: Ndesamburo hakuwa mbaguzi

Jeneza lililobeba mwili wa Philemon Ndesamburo likiongozwa na viongozi wa dini.
BAADHI ya viongozi wa dini, wamemtaja mbunge mstaafu wa Moshi Mjini, hayati Philemon Ndesamburo kama mtu asiyekuwa na makuu na rahisi kuwasiliana na kuonana naye, ikilinganishwa na watu wengine wenye nyadhifa katika maeneo mbalimbali.

Walimtaja Ndesamburo pia kama mfanyabiashara, aliyetumia utajiri wake na nafasi alizokuwa nazo kisiasa kwa ajili ya kusaidia makundi mengine ya kijamii wakiwamo, walemavu madhehebu ya dini, siasa, wafanyabiashara na mengineyo.

Akitoa salamu za Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya baraza hilo, Shehe Mlewa Shaaban alisema kwa kipindi ambacho amemfahamu Ndesamburo, alimuona kama mtu aliyejitoa katika kusaidia jamii zaidi.

“Mungu alimpa hayati Ndesamburo karama ya peke yake, kwa jinsi nilivyomfahamu hakuwa na makuu wala majivuno kwa kile alichonacho... wapo baadhi ya wafanyabiashara kwa jinsi walivyo ukitaka kumuona ni bora umtafute Mungu, unaweza kumuona, kuliko yeye,” alisema.

Shehe Shaban alitaka jamii nzima kuiga mambo mema, kama ambavyo yamefanywa na Ndesamburo wakati wa uhai wake. Awali akimzungumzia hayati Ndesamburo, Mwasisi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edwin Mtei alisema alikuwa kiongozi msikivu na mwenye mtazamo wa kuleta mabadiliko ya wananchi kiuchumi na kijamii.

“Nimefanya kazi na Ndesamburo hata miaka ile ya 1991 tunafanya harakati za kuleta mageuzi ya kisiasa, tulikuwa pamoja na alitumia fedha zake na muda ili kuona taifa linakuwa na mabadiliko ya kifikra ikizingatiwa tulikuwepo katika mfumo wa chama kimoja cha siasa,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alishauri jeshi la polisi kutotumika katika masuala ya kisiasa, kwani kwa kufanya hivyo ni kujenga chuki baina ya serikali na wananchi, jambo ambalo huenda likaathiri umoja wa kitaifa uliopo.

“Hii inasikitisha wananchi wanataka kumuaga mpendwa wao katika Uwanja wa Mashujaa... inafika usiku tunapokea barua kwamba haturuhusiwi kwa visingizio vya kuwepo kwa shule na mahakama, hili linaonesha dalili za ubaguzi wa wazi, tunajenga chuki... epukeni, tutaligawa taifa,” alisema.

Alitaka viongozi wa serikali akiwamo Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa na Rais Dk John Magufuli kulijenga taifa kwa misingi ya umoja. Nao mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliiomba serikali kulinda uhuru wa kidemokrasia badala ya kuuminya.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment