Kuwait yatoa bilioni 110/- ujenzi wa barabara Tabora

Rais John Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Ibrahim Al Najem alipofika kumtembelea Ikulu jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu). 
 
RAIS John Magufuli ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 51 (sawa na takribani Sh bilioni 110), kwa ajili ya kujenga barabara ya Chaya - Nyahua mkoani Tabora yenye urefu wa kilometa 85.

Barabara hiyo itaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mkoa wa Singida na Tabora. Rais Magufuli alitoa shukrani hiyo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam, alipofanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa nchini, Jasem Ibrahim Al Najem na kupokea msaada wa magari mawili ya kusombea taka ngumu yenye thamani ya Dola za Marekani 200,000.

Magari hayo yametolewa na Serikali ya Kuwait kwa lengo la kuunga mkono kampeni ya usafi hapa nchini. “Naomba unifikishie salamu zangu kwa Mfalme wa Kuwait, mwambie tunathamini mchango mkubwa wa Kuwait katika maendeleo ya nchi yetu, hizi fedha za barabara mlizotupatia zitatusaidia kumalizia sehemu hiyo ya barabara ambayo ndio ilikuwa imebaki,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia aliishukuru Serikali ya Kuwait kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za utoaji wa huduma za kijamii nchini, ikiwemo msaada wa Dola za Marekani 250,000 kwa ajili ya kununulia vifaa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na visima vya maji safi 27 vilivyochimbwa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya wanafunzi na wananchi wa maeneo jirani na shule.

Aidha, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa Dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya kuikarabati Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar. Pia aliiomba Serikali ya Kuwait kuweka alama ya kumbukumbu ya uhusiano wake na Tanzania kwa kusaidia ujenzi wa barabara za makao makuu ya nchi mjini Dodoma.

Alimhakikishia Mfalme wa Kuwait, Sheik Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Kuwait, hususani katika masuala ya kiuchumi, ikiwemo mafuta na gesi ambayo imevumbuliwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment