SERIKALI imetangaza kufuta ada ya leseni ya magari, kupandisha bei ya vinywaji baridi na bia, mafuta na kupunguza ushuru wa mazao unaotozwa na halmashauri za wilaya kutoka asilimia tano hadi tatu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitangaza hayo jana wakati akisoma Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 bungeni mjini hapa. Akizungumzia Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, alisema kuwa serikali inafanya marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia tano.
Hata hivyo, Dk Mpango alisema kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa kukuza uchumi wa viwanda, baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini hazitafanyiwa marekebisho hayo. Dk Mpango alieleza kuwa ushuru wa bidhaa kwenye viwanja baridi unapandishwa kutoka Sh 58 kwa lita hadi Sh 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh tatu kwa kila lita.
Aidha, ushuru wa bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje kutoka Sh 58 kwa lita hadi Sh 61 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh tatu kwa lita. “Aidha, ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 58 kwa lita,” alieleza.
Kuhusu ushuru wa bidhaa kwenye matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini, utashuka kutoka Sh 9.5 kwa lita na kuwa Sh 9.0 kwa lita. Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi nchini, kutoka Sh 210 kwa lita hadi Sh 221 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh 11 kwa lita.
Bidhaa nyingine zilizopanda ni ushuru wa bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka nchini na ambayo haijaoteshwa kutoka Sh 429 kwa lita hadi Sh 450 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh 21 kwa lita.
Aidha, ushuru wa bidhaa kwenye bia nyingine zote kutoka Sh 729 kwa lita hadi Sh 765 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh 36 kwa lita. Pia alitangaza kupandisha ushuru wa bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi ikijumuisha vinywaji vya kuongeza kutoka Sh 534 kwa lita hadi Sh 561 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh 27 kwa lita.
Aidha, ushuru wa bidhaa kwa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka Sh 202 kwa lita na kuwa Sh 200 kwa lita.
Ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka Sh 2,236 kwa lita hadi Sh 2,349 kwa lita (ongezeko la Sh 113 kwa lita).
Kuhusu vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka Sh 3,315 kwa lita hadi Sh 3,481 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh 166 kwa lita. “Aidha, ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini utabaki kuwa shilingi 3,315 kwa lita,” alieleza Dk Mpango.
Akizungumzia ushuru wa bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha asilimia 75 kutoka Sh 11,854 hadi Sh 12,447 kwa kila sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la Sh 593 kwa sigara elfu moja.
Pia serikali imeongeza ushuru wa bidhaa za sigara zenye vichungi kutoka Sh 28,024 hadi 29,425 kwa kila sigara 1,000, na ushuru wa bidhaa kwenye sigara zenye tofauti za zenye vichungi na zisizo na vichungi. Dk Mpango alisema ushuru wa bidhaa ya cigar unabaki kuwa asilimia 30.
Alitangaza serikali kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari iliyokuwa inalipwa hata kwa magari ambayo hayatumiki ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu. “Badala yake ada hiyo itatozwa kwa magari yanayotembea tu, kwa sababu hiyo, ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na taa utaongezeka kwa kiasi cha shilingi 40 kwa lita moja kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 379 kwa lita kwa mafuta ya petroli,” alisema na kuongeza:
“Kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi 255 kwa lita kwa mafuta ya dizeli na kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 425 kwa lita hadi shilingi 465 kwa lita kwa mafuta ya taa. “Lengo la hatua hii ni kuwaondolea wananchi usumbufu wa kudaiwa ada hii hata kwa magari ambayo hayatumiki.”
Dk Mpango alisema kuwa hatua za ushuru kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 27.80. Kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani, Dk Mpango alitangaza kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari ili ada hiyo ilipwe mara moja tu ili gari linaposajiliwa na baada ya hapo kulipiwa kupitia Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta ya petroli na dizeli, na mafuta ya taa.
“Aidha, serikali inatoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada hiyo yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma,” alitangaza Dk Mpango na kushangiliwa kwa kelele kubwa na wabunge ambao wengine walisimama na kuserebuka.
Badala yake, alipendekeza kuongeza ada ya leseni ya magari wakati wa usajili wa mara ya kwanza. Alitaja ongezeko la ada ya leseni za magari kuwa ni gari lenye ujazo wa injini ya 501-1500 cc kutoka kiwango cha sasa cha Sh 150,000 hadi Sh 200,000 (ongezeko la Sh 50,000).
Alisema gari lenye ujazo wa injini 1501 hadi 2500 cc kutoka kiwango cha sasa hadi Sh 200,000 hadi Sh 250,000, ikiwa ni ongezeko la Sh 50,000. Aidha, gari lenye ujazo wa injini 2501 cc na zaidi kutoka kiwango cha kiwango cha sasa cha 250,000 hadi Sh 300,000 ikiwa ni ongezeko la Sh 50,000.
“Hatua hizi ni pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 77,603.5,” alieleza. Kuhusu Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, alitangaza kupunguza ushuru wa mazao unaotozwa kwa halmashauri za wilaya kutoka asilimia tano ya thamani ya mauzo hadi asilimia tatu kwa mazao ya biashara na asilimia mbili kwa mazao ya chakula.
“Aidha, mtu anayesafirisha mazao yake kutoka halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani moja asitozwe ushuru. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wakulima kulipwa bei stahiki ya mazao yao na hivyo kuboresha mapato yao.
Hatua hii inatarajiwa kuhamasisha uzalishaji wa mazao,” alisema. Kuhusu Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), serikali imetangaza kusamehe VAT kwenye bidhaa za mtaji ili kupunguza gharama za ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo ya kuzalishia hivyo kuvutia wawekezaji katika sekta ya viwanda.
Aidha, alisema hatua hiyo itahusisha viwanda vya mafuta ya nguo, ngozi, madawa ya binadamu na mifugo. Aliongeza kuwa hatua hiyo pia itawezesha viwanda vidogo na vya kati kupata unafuu wa gharama za VAT kwa mashine na mitambo watakayonunua kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Jambo jingine zuri ambalo wabunge walilipokea kwa furaha na nderemo ni kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu kwa kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine hususan zisizo na bandari,” alieleza.
“Hatua hii itahamasisha wasafirishaji kutoka nchi jirani kupitisha mizigo yao kwa wingi kwenye bandari zetu na hivyo kukuza uchumi wa nchi kutokana na kuongezeka kwa mapato ya bandari.
“Vile vile kukua kwa sekta ya bandari kutachangia kuongezeka kwa ajira nchini.” Kwa wakulima, waziri alitangaza kusamehe VAT kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini, na pia kusamehe VAT kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji wa vifaranga na kukuza sekta ndogo ya ufungaji ili iweze kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa,” alieleza. Katika Sheria ya Kodi ya Mapato, alitangaza kupunguza Kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezaji atakapoanza uzalishaji.
Pia kusamehe Kodi ya Mapato kwa waunganishaji wa magari, matrekta na boti za uvuvi, lengo likiwa ni kuongeza ajira, kuongeza mapato ya serikali na pia kuhamasisha uhaulishaji wa teknolojia.
0 Maoni:
Post a Comment