Wamachinga washangilia

Wamachinga wakishangilia 

SHIRIKA la Umoja wa Wamachinga (Shiuma) Tanzania na wafanyabiashara wa maduka, wamepongeza uamuzi wa Serikali kutaka wafanyabiashara ndogo kusajiliwa ili watambulike na kutafutiwa maeneo bora kwa shughuli zao.

Mwenyekiti wa Shiuma, Matondo Masanja wa Mwanza na wafanyabiashara maarufu wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Elias Kiguha na Mugheko Chanchawa, walisema hatua hiyo itaongeza heshima na mapato ya wafanyabiashara hao, wenye maduka, pato la taifa na kuongeza ajira.

Walikuwa wakizungumza kuhusu hotuba ya mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18 iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Kiguha alisema anaunga mkono usajili wa wafanyabiashara ndogo utawawezesha kutambulika katika maeneo maalumu hali itakayowawezesha pia kufanya biashara yao na kulipia kodi, huku pia wakiepusha adha ya kuziba njia na maduka ya wafanyabiashara wanaolipa kodi.

Akapendekeza, “Ninashauri eneo la Soko la Kariakoo hadi DDC lijenge jengo kubwa la ghorofa hata 20 ili wamachinga wengi wapate maduka mle. Hii itaongeza ajira na kuwaondoa wamachinga wanaoziba barabara na maduka katika mitaa mingi Dar es Salaam.”

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Wamachinga alisema wanaishukuru Serikali ya Rais John Magufuli kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na Waziri Mpango kwa kupokea, kujadili na kuona umuhimu wa kuwatambua rasmi wafanyabiashara ndogo.

Naye Mugheko Chanchawa alisema kabla ya usajili huo, Serikali ilikuwa inapoteza mapato. “Wakisajiliwa wakalipa hata ushuru wa shilingi 500 kwa siku, taifa litapata pesa nyingi kuboresha huduma za jamii,” alisema
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment