Mratibu wa huduma za dharura wa shirika la
kimataifa la wahajiri amesema kuwa, nyumba zisizopungua elfu moja
zimeharibiwa na mafuriko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Kwa mujibu wa shirika la habari la
IRIB, mratibu huyo alitangaza habari hiyo jana na huku akiashiria
kuanza msimu wa mvua katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria na
kutokea mafuriko kwenye eneo hilo amesema, watu wasiopungua 43,000
wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na kuharibiwa na mafuriko.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ajenda kuu ya
shirika la kimataifa la wahajiri hivi sasa ni kuwatafutia makazi mapya
watu walioathiriwa na mafuriko hayo.
Mbali na majanga ya kimaumbile, wananchi wa Nigeria wanakabiliwa pia na mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram
Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni, Ofisi
ya Kuratibu Misaada ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ilisema mjini Lagos
Nigeria kuwa, mamilioni ya wananchi wa mikoa mitatu ya Yobe, Borno na
Adamawa ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wanahitajia misaada ya
haraka ya chakula, lakini kutokana na kukosekana fedha za kutosha,
mashirika ya misaada ya kibinadamu yamelazimika kufunga ofisi zao kwenye
mikoa hiyo.
Ripoti ya ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa
iliongeza kuwa, kukosekana fedha kumeathiri vibaya juhudi zote
zilizofanyika hadi hivi sasa na hivi sasa ripoti zinaonesha kuzidi kuwa
mbaya hali ya wakazi wa mikoa hiyo ambao wanashindwa kuendesha kazi zao
za kawaida kama vile kilimo kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo
mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi wa Boko Haram.
0 Maoni:
Post a Comment