WASHITAKIWA 15 wakiwemo 13 waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya Exim tawi la Jijini Arusha, wanaanza kujitetea siku tatu mfululizo kuanzia Juni 14 mwaka huu.
Washitakiwa hao wiki iliyopita walitiwa hatiani katika maamuzi madogo kuwa wana kesi ya kujibu pale waliposomewa na Hakimu Mfawidhi, Deudedit Kamugisha wa Mahakama ya wilaya ya Arusha/Arumeru Mkoani Arusha. Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne ikiwemo wizi wa dola za kimarekani 300,000 katika benki hiyo, kughushi, kuharibu nyaraka na utakatishaji fedha.
Akisoma uamuzi huo, Kamugisha alisema washitakiwa hao wote wana kesi ya kujibu kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyotolewa katika mahakama hiyo, hivyo wanapaswa kujitetea kuanzia Juni 14, 15 na 16 mwaka huu katika mahakama hiyo. Kamugisha alisema mashahidi 37 waliotoa ushahidi na vielelezo 20 vilivyowasilishwa katika mahakama hiyo vimeishawishi mahakama kuamini kuwa washitakiwa hao wana kesi ya kujibu, hivyo wanapaswa kujitetea kwa kula kiapo cha maandishi.
Alisema ushahidi umeonesha wazi kuwa watuhumiwa hao walishiriki kufungua akaunti na kufanikiwa kuiba dola taslimu au hundi mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Hakimu huyo alisema pia baadhi ya watuhumiwa katika kesi hiyo walihusika kuharibu nyaraka na kughushi ili kuhalalisha wizi walioufanya katika benki hiyo.
Alisema ushahidi ulionesha wazi kuwa dola zilichepushwa kwa kutoingia katika akaunti ya NCAA na kuingia katika akaunti sita binafsi zilizofunguliwa na baadhi ya watuhumiwa, lengo ni kutekeleza njama za wizi na kuiba dola zilizokuwa zikilipwa na mawakala wa utalii wanaotaka kupata huduma katika hifadhi ya Ngorongoro.
Uamuzi wa Hakimu Kamugisha unaungana na hoja za mawakili wa serikali kuwa watuhumiwa wote katika kesi hiyo ya kughushi, wizi wa kiasi hicho, kuharibu nyaraka na utakatishaji wana kesi ya kujibu kwa mashitaka waliyofunguliwa nayo na kutupilia mbali hoja za mawakili wa utetezi waliosema kuwa wateja wao hawana kesi ya kujibu.
Watuhumiwa katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Meneja wa benki tawi la Exim Arusha, Bimel Gondalia( 37), Lilian Mgaya (33) mshitakiwa wa tatu Neema Kinabo (30) ameachiwa baada ya kukiri kosa na kulipa faini na mshitakiwa na nne ni Livistone Julius (36).
Wengine ni pamoja na mshitakiwa wa tano Joyce Kimaro(36), mshitakiwa wa sita ni Daud Mosha, mshitakiwa wa saba ni Doroth Tigana(50), Evans Kashebo (40), mshitakiwa na tisa Mosses Chacha (37) ameachiwa baada ya kukiri kosa na kulipa faini ya Sh milioni 100 mshitakiwa wa kumi katika kesi hiyo Tuntufe Agrey (32). Mshitakiwa wa 11 ni Joseph Meck(34), Janes Massawe(32) mshitakiwa wa 12, mshitakiwa wa 13 ni Christopher Lyimo(34) na mfanyabishara wa Arusha Gervas Hugo ambaye ni mshitakiwa wa 14.
Washitakiwa wanne tu ambao ni Gomes mshitakiwa wa kwanza, mshitakiwa wa nane Kashebo, mshitakiwa wa 11 Meck na Lyimo wako nje kwa dhamana kwani hawakushitakiwa na shitaka la utakatishaji fedha, lakini washitakiwa wengine wote wako rumande kwa makosa ya utakatishaji fedha haramu. Kesi hiyo haina dhamana kwa mujibu wa sheria.
0 Maoni:
Post a Comment