WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Bulaya wa Bunda Mjini na Halima Mdee wa Jimbo la Kawe, wamepigwa marufuku kushiriki shughuli zozote za Bunge hadi Aprili 2018 baada ya kudaiwa kufanya fujo bungeni kwa kudharau mamalaka ya Bunge.
Licha ya kukosa uwakilishi wa wananchi katika majimbo yao, kwa adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao na shughuli za Bunge kuanzia jana huku Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti ukiwa umebakiza takriban siku 25, hawatahudhuria mikutano mingine miwili wa Nane, itakayofanyika Novemba mwaka huu na ule wa Tisa utakaofanyika Februari mwakani.
Kadhalika, wabunge hao watakosa posho yao ya kila siku ya kikao ambayo ni takriban Sh 220,000 na hawatahudhuria vikao vyoyote vya Kamati zao za Kudumu za Bunge pamoja na safari.
Wabunge hao wameadhibiwa kutokana na kuonesha utovu wa nidhamu bungeni baada ya Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) kutolewa kwa nguvu nje ya Bunge.
Katika sakata hilo wakati anatolewa Mnyika, Mdee alionekana kumkaba mmoja wa askari wa Bunge kwa kumvuta koti kwa nyuma huku Bulaya akihamasisha wabunge wengine wa upinzani kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge, kugomea adhabu hiyo, aliyopewa Mnyika.
Awali, wakati wa mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini, hasa wakati Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alipokuwa akichangia, wabunge wengi hasa wa upinzani, walikuwa wakisimama kutaka kumpa taarifa mbunge huyo ambaye katika mchango wake alijielekeza kuichambua hotuba iliyotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara hiyo, John Mnyika.
Katika hali hiyo, Mnyika aligoma kutii agizo la Spika Job Ndugai aliyemtaka kuketi hata baada ya kupewa onyo na hatimaye, Spika akaagiza atolewe nje kwa kutumia askari wa bungeni.
Mbunge huyo wa Kibamba alikuwa analazimisha taarifa yake ipokelewa kuhusu madai kwamba kuna mbunge alikuwa amemwita mwizi. Chanzo cha hali hiyo kilikuwani hatua ya wabunge wa upinzani kuiponda ripoti ya Kamati Maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli ya kuchunguza kontena 277 za makinikia zilizokuwa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikutane Jumamosi iliyopita na kuwataka wabunge hao wafike mbele ya Kamati. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Mkuchika alisoma maazimio yaliyofikiwa na kuwaomba wabunge wajadili kuhusu adhabu ilizopendekeza.
Kwa mujibu wa Kamati ya Mkuchika, ambaye ni Mbunge wa Newala (CCM), mapendekezo yao yalikuwa ni kutaka wabunge hao wasimame siku zilizobaki katika Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti unaoendelea, na Mkutano wa Nane isipokuwa wafike siku ya mwisho ya mkutano huo.
0 Maoni:
Post a Comment