Mdahalo wa urais mwaka 2013, kuanzia kushoto waliokuwa wagombea urais Abduba Dida, James Ole Kiapi, Uhuru Kenyatta, Peter Keneth, Musalia Mudavadi, Martha Karua, Raila Odinga na Paul Muite
Kamati andalizi inayoshughulikia midahalo ya wagombea urais kupitia runinga na vyombo vingine vya Habari nchini Kenya imetoa ratiba kuhusu midahalo hiyo itakavyofanyika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.
Itakuwa ni mara ya pili katika siasa za nchi hiyo kwa wagombea wa urais kukutana ana kwa ana katika mdahalo kuweka wazi ajenda zao na kujibu maswali.
Wachira Waruru Mwenyekiti wa Kamati hiyo ametangaza kuwa kutakuwa na midahalo mitatu.
Mdahalo wa kwanza utakuwa kati ya wagombea urais pakee yao utakaofanyika tarehe 10 mwezi Julai kuanzia saa moja na nusu jioni saa za Afrika Mashariki.
Wagombea wenza nao watakuwa na siku yao tarehe 17 mwezi Julai, huku mdahalo wa tatu na wa mwisho ukiwakutanisha tena wagombea urais tarehe 24 mwezi uo huo wa Julai.
Wakati uo huo, Tume ya Uchaguzi nchini humo imetangaza kuwa wagombea wote wa urais 18 wawasilishe vyeti vyao tarehe 28 mwezi huu.
Wagombea hao ni pamoja na Profesa Michael Wainaina mgombea binafsi, Peter Ondeng -chama cha Restore and Build Kenya Party, Abduba Dida - Tunza Coalition, Kennedy Mongare – chama cha Federal Party of Kenya.
Ekuru Aukot - Thirdway Alliance Party, Joe Nyagah -Mgombea binafsi, Nazlin Omar - Mgombea binafsi, Cyrus Jirongo- UDP, Uhuru Kenyatta - Jubilee , Raila Amolo Odinga ODM kupitia muungano wa NASA.
Wagombea wenine binafsi ni pamoja na: David Munga, Stephen Oweke Oganga,Robert Mukwana Juma,Joseph Ngacha, Japheth Kavinga, Nixon Kukubah,Joseph Musyoka, Erastus Nyamera.
Licha ya wagombea hawa, ushindani mkubwa ni kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ambao pia walipambana mwaka 2013.
0 Maoni:
Post a Comment