Waliofukuzwa Msumbiji wafikia 193

 

IDADI ya Watanzania wanaorudishwa nchini kutokea nchi jirani ya Msumbiji imeendelea kuongezeka hadi kufikia watu 193 ilipofika jana jioni.

Mwandishi wa gazeti hili alishuhudia makundi ya Watanzania hao wakiingia kupitia mpaka uliopo Kijiji cha Kilambo mkoani hapa.

Taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mtwara, Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Rose Mhagama, zimesema kuwa hadi jana kulikuwa na Watanzania 193 waliopokelewa kutoka Msumbiji kwa kupitia katika Kijiji cha Kilambo wilayani Mtwara.

Mhagama alisema kundi la kwanza la watu 58 lilipokelewa siku tatu zilizopita, likafuatiwa na kundi la Watanzania wengine 122 waliopokewa juzi na jana walipokelewa 13 na hivyo kufanya idadi hiyo kufikia 193 waliofukuzwa nchi hiyo jirani yenye uhusiano wa kindugu na Tanzania.

Alisema ofisi yake hivi sasa inahakiki utanzania wao na baadaye kuwasaidia kuwarudisha kwao kulingana na taarifa watakazopata na kuzihakiki kwa kuwa licha ya kudai kuporwa hati zao za kusafiria, wapo baadhi wanaokumbuka namba na hivyo wanaziingiza katika mfumo ili kuzitambua.

Gazeti hili lilikuwepo kijijini Kilambo lilishuhudia watanzania hao wakiingia kwa makundi ya watu watatu au wanne kwa kutumia usafiri wa ngalawa na wengine kivuko cha Mv Kilambo na kupokelewa na maofisa uhamiaji na kuwahoji kisha kuwasafirisha hadi mjini Mtwara kwa taratibu zingine.

Kwa mujibu wa Watanzania hao waliosombwa na msako huo, wanadai kuwa kinachofanyika huko ni unyanyasaji na uporaji wa mali na fedha za wageni unaondeshwa na polisi kwa kisingizio cha wahamiaji haramu.

Walidai kuwa katika msako huo wakibaini ni Mtanzania, unapororwa kila kitu simu fedha gari na kuchukuliwa mikono mitupu na watoto wako na kutupwa mahabusu hadi siku ya kupelekwa nchini kwao.
Walidai kwa wengi waliyoko nchini humo ni wafanyabiashara ambao hivi sasa wapo maporini kwa sababu pamoja na kuporwa mali pia wakikamatwa wanadhalilishwa sana kwa vitendo vya kikatili.

Rashidi Yasini mkazi wa mkoani Ruvuma ambaye alijitambulisha kuwa amekuwa akifanya biashara ya duka nchini Msumbiji kwa miaka kadhaa sasa, alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa siku mbili kisha kurudishwa nchini akiwa mikono mitupu na wala hajui familia yake inaendeleaje huko.

Yasini alisema alikuwa anafanya biashara kitongoji cha Nanyupu Wilaya ya Mtepwezyi Mkoa wa Pemba ambako ni jirani na machimbo ya madini katika eneo linalodaiwa kumilikiwa na mwekezaji wa kizungu ambaye alidai ndio magari yake yametumika kuwasafirisha hadi mpakani mwa Msumbiji na Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kilambo, Mohamedi Mkama, alisema wamekuwa wakiwapokea Watanzania wanaotoka Msumbiji, lakini hii ni tofauti maana mara zote huwa wanaletwa chini ya ulinzi na kukabidhiwa kwa maofisa Uhamiaji wa huku kwetu.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda alisema watahakikisha Watanzania hao wanatafutiwa usafiri wa kuwafikisha makwao kwa waliyo tayari, lakini wale wanaotaka kusubiri kujua hatima ya mali na familia zao huko Msumbiji hawatalazimishwa.

Jijini Dar es Salaam, serikali imesema suala la kufukuzwa kwa Watanzania waliokuwa wakiishi Msumbiji katika mji wa Monte Puez Jimbo la Cabo Delgado zinaweza kuwa limetokana na kuingia bila kufuata sheria ama baada ya kuingia kuvunja sheria na taratibu za ukazi na kufanya kazi bila kibali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira alisema hayo jana jijini Dares Salaam na kuwasihi waandishi wa habari kuziangalia taarifa hizo ili zisiwe chanzo cha kuleta matatizo baina ya nchi na nchi.

Alisema kama nchi isingependa kuingia kwenye mgogoro wowote na nchi jirani kwa kuwa kurudishwa kwao sio jambo geni, kwani kila nchi ina haki ya kufanya hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Msumbiji nchini, Ofisa Ubalozi, Maneno Wadyeko alisema ubalozi huo hauna taarifa yoyote rasmi ambayo kuhusu tukio hilo.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment