SERIKALI imesema Watanzania wanane waliokamatwa nchini Malawi, si majasusi wa serikali ya Tanzania, bali ni wafanyakazi wa Taasisi ya misaada ya Caritas iliyo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Songea mkoani Ruvuma.
Watanzania hao ambao kwa sasa wanashikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini humo, walikamatwa hivi karibuni kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana, chombo kimoja cha habari cha Malawi kilitoa taarifa hiyo kwa mara ya kwanza, kikidai kuwa watu hao walitumwa na Serikali ya Tanzania.
Kilidai walitumwa kuchunguza kama Serikali ya Malawi, inatengeneza silaha za nyuklia kwa kutumia madini ya urani ya kutoka katika mgodi huo.
Baada ya kupatikana kwa taarifa hiyo, Wizara hiyo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, ulifuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Baada ya kufuatilia, ilibainika kuwa ni kweli ni Watanzania kutoka katika taasisi hiyo ya Kanisa Katoliki.
“Watanzania hao walikamatwa na vyombo vya usalama katika wilaya ya Karonga, Malawi ambayo inapakana na Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya. Baada ya kukamatwa walifunguliwa kesi kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia eneo la mgodi bila kibali,” ilieleza taarifa hiyo jana.
Ilieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, uliwasiliana na taasisi ya Caritas, kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao kufanya ziara nchini humo.
“Ubalozi ulielezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo walitaka kufahamu juu ya madhara yatokanayo na machimbo ya madini ya urani. Watanzania hao kwa sasa wapo katika Gereza Kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 4 Januari 2017,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ubalozi huo unaendelea kufanya mawasiliano na Kanisa Katoliki Songea ili kupata maelezo zaidi kuhusu ziara ya watu hao, kwa madhumuni ya kuyawasilisha katika mamlaka husika ili watuhumiwa waweze kutolewa.
Aidha, Wizara kupitia Ubalozi huo imebaini kuwa taasisi hiyo ya Caritas, iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini Malawi bila kupata kibali kutoka mamlaka husika na bila kutoa taarifa katika Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara hiyo.
Taarifa hiyo pia ilifafanua kuwa kipindi cha kufanya ziara hiyo nchini Malawi, hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya Malawi wanakuwa katika likizo ya mwaka kuanzia Desemba 22 hadi Januari 3, mwakani.
Hatua hiyo imeelezwa kukwamisha juhudi za kuwafuatilia watu hao, ikiwa ni pamoja na kukwamisha maombi ya kibali cha kuwatembelea watu hao juzi. Hata hivyo, Wizara hiyo kupitia Ubalozi nchini humo, inaendelea na jitihada za kuhakikisha suala la watu hao linapata ufumbuzi wa haraka.
Wizara hiyo imetoa mwito kwa taasisi za dini, vyuo vya elimu na watu binafsi, kuomba vibali na kufuata sheria za nchi nyingine, wanapofanya ziara za mafunzo au nyingine, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ofisi za Balozi kwa ajili ya kufahamisha taratibu zinazotakiwa kufuatwa, kabla ya kufanya ziara ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Gazeti hili jana lilimtafuta Mkurugenzi wa Caritas Jimbo la Songea, aliyetajwa kwa jina moja la Georgina ambaye namba yake ya simu imesajiliwa kwa jina la Agnec Malato. Mtu huyo alimtaka mwandishi amtafute Padri Kelvin Ngondola, kwa kuwa yeye si msemaji wa jimbo hilo.
0 Maoni:
Post a Comment