WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema kwamba kuanzia wiki ijayo wizara yake itawatangaza hadharani watu wote ambao wamekwepa kulipa kodi ya ardhi na majengo, wakiwemo vigogo walioko serikalini.
Akifungua semina juu ya jukumu la vyombo vya habari katika kutoa elimu ya sheria, kanuni na taratibu katika utawala wa ardhi ili kusaidia kutatua migogoro, iliyofanyika mjini hapa, Lukuvi alisema kwamba watayatangaza majina hayo ili watu wawajue watu wanaojenga majumba ya kifahari lakini hataki kulipa kodi ya serikali.
“Tutatangaza majina yao halisi sio yale ya bandia, ili watu wawajue kuwa kuna watu wamejenga majumba ya fahari, lakini hawalipi kodi ya serikali, baada ya kutangaza tutawapiga faini. Na mwakani tutaweka kodi kubwa zaidi kwa mashamba na viwanja visivyoendelezwa,” alisema Lukuvi.
Alisema gharama ya kodi, pia imepunguzwa kutoka Sh 1,000 na sasa mtu atalipia ekari moja kwa Sh 400. “Nani huyo asiyeweza kulipia kiasi hicho cha fedha,” alihoji.
Alisema wizara yake inaangalia hata wale ambao wanamiliki kimila, nao wachangie kidogo, kwa sasa hawalipii hata kidogo Kuhusu hoja ya kuwanyang’anya watu mashamba ambayo hayajaendelezwa, alisema serikali haitaangalia cheo, jina wala wadhifa wa mtu, badala yake wale wote wenye mashamba ambayo hajaendelezwa watanyang’anywa.
Alisema kama kuna kiongozi yeyote serikali au kigogo mstaafu, ambaye amehodhi ardhi katika mkoa wowote na hajaiendeleza, huyo atahesabiwa amekiuka masharti ya kumilikishwa ardhi na hivyo lazima achang’anywe.
Alisema kabla ya kufuta hati ya umiliki, Serikali inatoa notisi ya kufuta kabla ya kufanya hivyo kwa viwanja na mashamba, sasa mchakato ukiiva baada ya siku 90 kama utetezi wake hauridhishi, anampelekea rais anafuta hati hizo za umiliki.“Hakuna atakayepona katika mpango huu,” alisema Lukuvi.
Alishauri taasisi za serikali kutumia wapima ardhi binafsi kwani ni waadilifu kuliko wale wa serikali, “Wapima binafsi ni waadilifu, mkiwapa kazi maeneo yetu yatapona, mkiwapa viwanja 1,000 watakurudishia viwanja vyote, ila aliyeajiriwa na halmashauri atakurudishia viwanja 500, viwanja 500 ‘atavipiga’. Na ‘upigaji’ wao ni ufundi haswa.”
Hata hivyo alisema kwa sasa upigaji umepungua wizarani kwake.
“Hakuna siri, wizi hakuna, ujambazi, rushwa zimepungua sana, mtu akiniambia ameombwa rushwa pale wizarani nitamshangaa, tunataka iwe wizara salama inayotoa hati kwa haraka,“ alisema. Miaka 10 nchi yote iwe imepangwa, kupitia kanda nane ili kuepusha watu wote kwenda makao makuu ya wizara kwa ajili ya kufuatilia hati kusajiliwa.
“Ilikuwa ni kama bahati kupata hati, lakini leo tumeweka mfumo, kwamba kila mtu aliyelipia ada zake zote apewe hati ndani ya mwezi mmoja”, alisema.
Alisema katika kufanikisha upimaji wa kila kipande cha ardhi, fedha zinazotolewa na wafadhili tu, haziwezi kufanikisha azma hiyo ya Serikali. Hivyo, alisema bado wanashauriana namna ya kuanzisha mfuko maalumu, ambao fedha zake zitatumika kwa ajili ya kupanga na kupima kila kipande cha ardhi.
Ili kurahisisha kazi ya mipango miji, serikali imeamua kukabidhi kazi hiyo kwa kampuni binafsi. Alisema tayari kampuni 33 za upangaji miji na kampuni 63 za upimaji, zimesajiliwa na bodi zao ili ziweze kufanya kazi ambayo ingefanywa na serikali “Serikali peke yake haiwezi, haina wataalam wa kutosha,” alisema.
Alisema kuna sehemu wameweza kutoa hati kwa siku tatu, “tunataka tufike mahali ufike wakati tutoe hati ndani ya siku moja,” alisema.
Akizungumzia master plan, Lukuvi alisema kuna rasimu nane ambazo zimekamilika mwaka huu za miji mbalimbali na sasa wako kwenye hatua ya kusikiliza maoni ya wananchi ili miji hiyo iweze kuzaliwa upya.
Alisema ‘master plan’ ya jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa mipango, itakayokamilishwa mwakani ili kuwe na mpango mpya wa kuendeleza majiji na miji mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam.
Waziri huyo pia alisema katika maeneo ambayo yamejengwa holela, kuna mpango wa urasimishaji katika maeneo yote ambayo hayakupangwa wala kupimwa, Serikali itayarasimisha. Mwaka huu tayari Serikali imetoa hati 124,000 katika nchi nzima.
Alitoa mfano wa maeneo hayo ni Kimara, Chasimba, Makongo na Goba. Lukuvi alsema wizara yake pia inaandaa sheria ya kuwatambua madalali na kuweka sifa za madalali hao, pia sheria hiyo italinda haki za mpangaji na mmiliki wa nyumba.
“Kuna madalali matapeli, wanaghushi hata mihutasari ya mahakama na kwenda kubomoa nyumba za watu, sasa tunatunga sheria kufahamu ni nani anastahili uwa dalali, sio unaamka tu unaweka kibao unadai wewe ni dalali,” alisema.
Kuhusu wapangaji alisema sheria hiyo itawasaidia wasipandishiwe kodi kiholela na wenye nyumba, lakini pia wamiliki wa nyumba watalindwa na sheria hiyo katika kulinda haki zao.
Kuhusu ujenzi wa nyumba, alisema licha ya shirika la nyumba na kampuni zingine kuendelea kujenga nyumba kwa ajili ya makazi, lakini wizara yake bado inatafuta teknolojia ambayo itasaidia nyumba za bei nafuu ziweze kujengwa kuliko ilivyo sasa hivi.
0 Maoni:
Post a Comment