Naibu Waziri awapa wiki 2 watumishi wa Ngorongoro



NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani ametoa wiki mbili na siku tano kwa watumishi wote wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wenye mifugo na majengo ya kudumu ndani ya eneo la hifadhi hiyo, kuorodhesha majina yao.

Hatua hiyo ya kuorodhesha, wataifanya kwa uongozi wa mamlaka hiyo na kusalimisha taarifa ya kile wanachokimiliki ndani ya eneo hilo, ikiwa ni utekelezaji maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa hivi karibuni kwa uongozi wa mamlaka hiyo.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo, mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na Ngorongoro. Kikao hicho kilifanyika kwenye makao makuu ya NCAA wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.

Makani alisema baadhi ya maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu ambayo yameshaanza kufanyiwa kazi ni kuondolewa mifugo yote maeneo ya Kreta, kuhakikisha upatikanaji wa maji na chumvi kwa ajili ya mifugo na wananchi, idadi ya mifugo kutambuliwa na kupigwa chapa na kutambua idadi ya wananchi ndani ya eneo la mamlaka na kupewa hati za utambuzi.

“Mpaka ikifika tarehe 15 Januari, kila mtumishi ambaye yeye binafsi ana mifugo ndani ya eneo hili, maana tunaanzia nyumbani, Conservator (Mhifadhi) uweke utaratibu wa kupokea taarifa kutoka kwao, kila mmoja aweze kudeclare (kutangaza) umiliki wake wa mifugo ndani ya eneo la hifadhi, ng’ombe, mbuzi, kondoo.

“Lakini pia kila mtumishi ambaye ana nyumba ya kudumu ndani ya hifadhi, iliyojengwa kwa matofali, mabati, zege na kadhalika atuambie, na mimi nishauri tu kuwa muwazi itakusaidia. Kwa sababu haiwezekani sisi tuanze kuwaambia watu wengine, wewe kwa nini umejenga nyumba ya kudumu hapa, wakati tunapowaonesha vidole na wengine sisi tunazo, hatuwezi kwenda kuwaambia wengine, wewe kwanini una mifugo humu 200,000, 2000, 1000 au 500 wakati wengine sisi humu tuna mifugo zaidi yao hata mara mbili”, alisisitiza Makani.
Alisema kuwa kwa wale waajiriwa wapya, wapewe elimu juu ya malengo na majukumu mahsusi ya taasisi hiyo na miiko yake, ambayo ni pamoja na uwepo wa maeneo maalumu ya uhifadhi yasiyoruhusiwa mifugo na majengo ya kudumu.

Aliwataka watumishi wa mamlaka hiyo, kusoma kwa makini madhumuni ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo na majukumu mahsusi iliyopewa ili kufanya vizuri zaidi katika uhifadhi endelevu wa hifadhi hiyo.

Kwamba watambue kuwa wao ndio wenye jukumu la kwanza la kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inastawi. Katika hatua nyingine, Makani ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa NCAA, kumkabidhi taarifa ya mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu.

“Zile wiki mbili nilizozisema ule mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya waziri mkuu, sina maana kwamba tutaanza kutekeleza kwenye wiki mbili, hivi tunavyoendelea kutekeleza kwa maana yapo mambo mengine hapa utekelezaji wake ni wa muda zaidi ya hizo wiki mbili, nataka nipate mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo hayo tuujadili na kuufanyia kazi kwa haraka,” alisema.

Alisema miongoni mwa changamoto kubwa za uhifadhi katika eneo hilo kwa sasa ni wingi wa mifugo na majengo ya kudumu ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, jambo lililohatarisha uhifadhi endelevu wa hifadhi.

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Freddy Manongi alisema jukumu kuu la kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ni kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori na malikale, utalii na jamii iliyopo ndani ya eneo la mamlaka hiyo.

Akizungumzia changamoto, alisema kuna uhaba wa chakula kutokana na wananchi wa eneo hilo kuzuiliwa kulima kisheria, malalamiko kuhusu wanyama wakali kuwashambulia wananchi na ongezeko la magonjwa mbalimbali huku mengi yakisababishwa na muingiliano wa wananchi na wanyamapori.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment