Mamlaka ya Mawasiliano Nchini Tanzania (TCRA) , jana December 14 imefanya Ukaguzi wa mwisho, kujiridhisha na kuruhusu Kituo cha Utangazaji cha Radio5 Arusha kurudisha Matangazo yake hewani ifikapo December 16 mwaka huu 2016.
Akiongea na Viongozi na baadhi ya Wafanyakazi wa Radio 5 baada ya kukamilisha ukaguzi wao, Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA Bw. Fredrick Ntobi alisema wao kama Mamlaka Waliamua kuja kufanya ukaguzi wao kwa ajili ya kujiridhisha kurudisha Matangazo ya Kituo hicho hewani December 16 ambapo ndiyo tarehe rasmi ya kuisha kwa adhabu waliyokuwa wametoa kwa kituo hicho.
Kituo cha Radio 5 kilisimamishwa na TCRA kurusha matangazo yaketoka tarehe 16 September 2016 kwa kukiuka baadhi ya kanuni.
Mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi wa Studio ya Kurusha Matangazo (On air Studio), Studio ya kuzalisha Vipindi (Production Studio), Chumba cha Habari (News room), Control Room, ofisi zote za Kituo pamoja na Mnara wa Kurushia Matangazo ambapo kote wamekuta kila kitu kiko sawa kwa kazi kama Mamlaka inavyotaka.
Hata hivyo Bw. Fredrick Ntobi akiwa ameongozana na Viongozi wa TCRA kanda ya Kaskazini, aliwakumbusha Watangazaji na Waandishi kufuata Maadili ya uandishi wa habari ili kulinda Vituo vyao na Kulinda taaluma zao kwa ajili ya kuendelea kuhabarisha na kuelimisha Jamii nzima ya Watanzania.
“Mimi niwasisitize tu kuendelea kufuata maadili ya taaluma yenu ya uandishi wa habari, kufuata sheria na kanuni za uandishi wa habari ambao mmesomea, tumieni lugha Sanifu ambayo inakubalika kwa jamii na tasnia yenu na niwatakie maandalizi mema ya kurudi hewani pamoja na Sikukuu zinazokuja”. Alimaliza kwa Msisitizo Bw. Fredrick Ntobi.
Hata hivyo kwa upande wa Mkurugenzi wa Tan Communication Media inayomiliki kituo cha Radio5, Bw. Robert Francis, aliwataka Wasikilizaji wa Radio5 kukaa mkao wa Kuhabarika, Kupata Burudani na kuelimika zaidi kupitia Radio5 kwani Wamejipanga vyakutosha kurudi hewani kwa Kishindo.
“Mimi niwaombe tu wasikilizaji wetu ambao najua wametumiss sana, wakae tayari Kuhabarika, kuelimika na kuburudika zaidi sababu mimi na Wafanyakazi wangu tumejipanga vya kutosha haswa ukizingatia kwamba mwaka mpya ndo huu unakuja.
"Kingine niwape pole tu wasikilizaji wetu wote kwa kutotusikia hewani kwa kipindi cha miezi mitatu, pamoja na Wadau ambao tumekuwa tukishirikiana kwa pamoja katika mambo mbali mbali niwaambie tu tunarudi rasmi Ijumaa ya tarehe 16 December 2016”. Alisema Mkurugenzi wa Radio5 Robert Francis.
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
0 Maoni:
Post a Comment