MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameagizwa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa kuendelea kuchunguza gharama za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya
ya Monduli iliyojengwa kwa fedha nyingi za serikali.
Hospitali hiyo ambayo imejengwa kwa fedha za serikali kwa gharama ya
Sh bilioni 2.7 ambapo haina jengo la upasuaji karibu na wodi ya wazazi
pamoja na maabara.
Waziri Mkuu alisema hospitali hiyo itasaidia kutatua changamoto za
afya kwa wananchi, lakini alishangaa ni kwa nini gharama za ujenzi huo
kuwa kubwa na kumwagiza Gambo kuendelea na uchunguzi juu ya fedha hizo
ili kujua kama kweli fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa
hospitali hiyo au la.
“RC endelea na uchunguzi wa fedha hizi za serikali wewe na timu yako
uliyoiunda ili kubaini je, ni kweli fedha hizi zimetumika kujenga
hospitali hii au la maana gharama za ujenzi ni kubwa kuliko uhalisia wa
hospitali hii,” alisema.
Aliagiza wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaoza watoto wa kike,
kwani serikali ikibaini kuwa kuna mzazi au mlezi kaoza mtoto wake au
kashiriki kupeleka posa atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo
kifungo cha miaka 30 jela.
Awali Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Zaveri Benela akisoma taarifa ya
hospitali hiyo, alisema licha ya kujengwa majengo hayo na serikali
kutoa fedha, lakini inakabiliwa na ukosefu wa jengo la upasuaji karibu
na wodi ya wazazi kwani bado wanasafirisha wagonjwa kwa zaidi ya mita
300 hadi kwenye jengo la upasuaji kwenye majengo ya zamani.
Pia kukosekana kwa jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara
kwenye majengo hayo, hali inayosababisha huduma hiyo kutolewa kwenye
maeneo miwili tofauti kwa wakati mmoja yaani wodi mpya na majengo ya
zamani na hali hiyo inaleta usumbufu kwa wagonjwa.
Alisisitiza kuwa ujenzi wa jengo la upasuaji na jengo la wagonjwa wa
nje ulikuwepo kwenye awamu ya pili wa ujenzi wa hospitali hiyo mpya
ambapo halmashauri iliomba fedha mwaka jana bila mafanikio.
Alisema wilaya hiyo ya Monduli ina jumla ya vituo vya kutolea huduma
za afya 41, zahanati 37, vituo vya afya vitatu na hospitali moja ya
wilaya, lakini bado wana upungufu wa watumishi wa afya 391 katika kada
mbalimbali.
Ujenzi huo mpya wa hospitali ya wilaya ulianza Machi, 2013 kwa
makandarasi wawili kupewa kazi ya ujenzi wa majengo hayo na mkandarasi
wa kwanza ni Meero Contractors aliyepewa Block A kwa jumla ya Sh
1,482,993,072.20 na mkandarasi wa pili Bullem Investment alipewa Block B
kwa jumla ya Sh 1,438,683,300.00.
Alisema majengo hayo miwili yana jumla ya wodi nne zenyewe vitanda
128, vyumba vya kujifungulia vitatu, vyumba vya watoto wachanga na
wanaozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) viwili.
0 Maoni:
Post a Comment