Msajili
wa Hazina nchini, Lawrence Mafuru amesema benki nchini zinashindwa
kueleza ukweli juu ya kuyumba kwao na kwamba madai ya kuwa hali zao ni
mbaya kutokana na agizo la serikali la kutaka fedha zake zitunzwe Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), hazina ukweli.
Mafuru
amesema taarifa ambazo serikali wanazo ni kwamba benki hizo zaidi ya 50
zimekopesha fedha nyingi kwa watu mbalimbali, lakini marejesho ya
madeni hayo yamekwama kiasi cha kusababisha benki hizo ziwe katika hali
hiyo.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Msajili wa Hazina licha ya kukiri kuwa mzunguko wa fedha umepungua kutokana na Tanzania kuchagua
kwamba fedha inazozipata zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya
matumizi ya kawaida, benki zinazolalamika zimeshindwa kurejesha fedha
ilizokopesha watu na taasisi mbalimbali.
Akizungumzia
taarifa zinazoenezwa kwamba benki zimekosa fedha za kujiendesha, Mafuru
alisema taarifa walizozipata ni kwamba Septemba mwaka huu, benki hizo
zaidi ya 50 nchini zimekopesha zaidi ya Sh trilioni 16.3 kwa watu
mbalimbali.
Hata
hivyo, alisema kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.43 zimekopeshwa bila
ya kurudishwa katika benki husika na kwamba benki hizo zinashindwa
kueleza ukweli uliopo badala yake wanalalamika kwamba hatua ya serikali
kuamua fedha zake zitunzwe BoT badala ya katika benki za kibiashara,
ndio sababu ya hali yao (benki) mbaya.
Kwa
mujibu wa Mafuru, serikali imeamua kuchukua uamuzi huo wa kuzitoa fedha
zake kutoka katika benki mbalimbali za kibiashara nchini kwa ajili ya
kuwezesha serikali kujua mapato wanayopata kutoka katika taasisi zake.
Msajili
wa Hazina amesema zaidi ya Sh bilioni 515 zimeingizwa BoT baada ya
uamuzi huo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao ulitangazwa na Rais John
Magufuli baada ya kushika madaraka mwaka mmoja sasa.
Mafuru
alikiri kuwa ni kweli kwamba mzunguko wa fedha umekuwa mdogo na kueleza
kuwa chanzo chake si kwamba benki zimekosa fedha kwa ajili ya
kujiendesha.
Alifafanua
kuwa awali watu wengi walitegemea safari na posho ambazo baada ya
chenji kubaki, walikuwa wakitumia bila ya malengo, lakini sio kwamba
mzunguko huo wa fedha unawaathiri watu wote.
“Tumeona
tusitegemee wahisani badala yake tujiwekeze katika miradi mikubwa ya
maendeleo ambayo kwa sasa haitaonekana, lakini baadaye itasaidia kuondoa
nafasi iliyopo sasa,’’ alisema Mafuru.
“Tayari
shilingi bilioni 515 zimeingizwa BoT na mpaka Septemba mwaka huu fedha
hizo zilikuwa kwenye akaunti hiyo. BoT ni sehemu ya mfumo wa benki,
kwani itakuwa inafanya kazi ya kukopesha kama zilivyo benki nyingine,” alifafanua Mafuru ambaye ofisi yake inasimamia mashirika na taasisi za umma.
Alifafanua
kuwa ofisi yake ambayo ina jukumu la kusimamia mapato na matumizi,
awali walikuwa wanapata shida kupata taarifa za mapato na matumizi
katika benki hizo zilizopo kila kona nchini na kwamba baada ya BoT
kuchukua dhamana hiyo, imewasaidia, kwani wanaandika barua na kupatiwa
taarifa hizo kwa muda mfupi.
Alisema
serikali inategemea mapato yake kutoka katika makundi matatu ambayo ni
Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na kupitia mashirika na taasisi
mbalimbali.
Alisisitiza
kuwa itasaidia kujua mashirika hayo zaidi ya 260 namna wanavyotumia
fedha zake katika miradi mbalimbali na kwamba suala la kuchukua fedha
bila ya kuzitumia lisiwepo.
0 Maoni:
Post a Comment