WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
ameagiza wananchi wote wanaomiliki viwanja vya makazi kuhakikisha
wanachukua hati za umiliki ifikapo Machi 30, mwakani.
Pia amemuagiza mwekezaji wa mgodi eneo la Maganzo wilayani hapa
kuwalipa fidia wananchi wanaomiliki mashamba na wenye nyumba walipwe
fidia zinazofanana na thamani ya nyumba zao.
Ametoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara
wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, ambako alisikiliza na kutatua kero
za wananchi kuhusu sekta hiyo.
Lukuvi alisema serikali imedhamiria kutatua kero za ardhi na ina
mkakati wa kuwasaidia wananchi wawe na hati halali za viwanja
wanavyomiliki huku akiwaahidi kupata hati zao ndani ya mwezi mmoja kwa
atakayelipia mapema.
Akizungumza na wananchi mjini Mhunze, Lukuvi alisema suala la hati ni
la lazima na kuwa inamsaidia mwananchi kuwa na usalama na kiwanja chake
na kupata huduma mbalimbali kama mikopo ya benki.
Katika hatua nyingine, amemwamuru mwekezaji wa mgodi eneo la Maganzo
kuwalipa fidia inayoendana na thamani za mashamba na nyumba wakazi
waliofika kutoa kero kwake, huku akiwataka wananchi hao kuendelea
kuyatumia mashamba hadi pale mwekezaji huyo atakapowalipa fidia huku
akionya vitendo vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wawekezaji waliopewa
vibali vya kuchimba madini kutumia nguvu zao vibaya.
Awali akizungumza na watumishi wa Halmashauri na Kamati ya Ulinzi na
Usalama Wilaya, Lukuvi aliwapongeza kwa kutokuwa na migogoro mingi ya
ardhi ukilinganisha wilaya zingine alizotembelea.
Aliiagiza Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kuongeza kasi ya upimaji viwanja na mipango miji.
0 Maoni:
Post a Comment