WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya
Monduli, Idd Kimanta kumaliza mgogoro wa Ardhi wa Kijiji cha Emairete
kilichopo Monduli Juu mkoani Arusha ambao umedumu kwa miaka 20.
Mgogoro huo ni wa shamba kubwa ambalo linamilikiwa na Kampuni ya Bia
Tanzania ambalo baadaye shamba lilirudishwa kijijini, lakini viongozi wa
zamani wa kijiji hicho walijimilikisha kinyemela.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kusimamishwa njiani katika
kijiji hicho na wananchi waliokuwa wamebeba mabango ya kumuomba msaada
wa kutatuliwa mgogoro huo akiwa anatoka nyumbani kwa Edward Moringe
Sokoine alipokwenda kuwasalimia wajane wa Sokoine pamoja na kuweka shada
la maua katika kaburi hilo.
Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Wilaya kutoa majibu ya kwa nini uongozi
wa wilaya umeshindwa kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye alifika kijijini hapo na
kutoa maelekezo.
Akijibu hoja hiyo, Kimanta alikiri kuwepo kwa mgogoro huo kwa miaka
20 na kwamba Waziri Lukuvi alitoa maelekezo ambayo halmashauri
inayafanyia kazi na kwamba imeshindwa kuleta majibu kwa wananchi hao
kutokana na ziara ya Waziri Mkuu.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu alitoa siku saba kwa mkuu huyo wa
wilaya kuhakikisha wanashughulikia mgogoro huo kwa kutekeleza maagizo ya
waziri wa ardhi.
“Natoa siku saba kuanzia leo uhakikishe mnatekeleza maagizo ya Waziri
wa Ardhi juu ya mgogoro huu ili wananchi waweze kupata haki yao ya
msingi,” alieleza Majaliwa.
Baada ya maelekezo hayo, aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na
imani ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli ambayo ipo kwa
ajili ya kusaidia wananchi wanyonge.
Awali akizungumza na wajane wawili pamoja na watoto wa marehemu
Sokoine alikokwenda kuwajulia hali, Waziri Mkuu Majaliwa alisema
serikali itaendelea kuenzi mema yote yaliyofanywa na Waziri Mkuu huyo
aliyefariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro, Aprili 12, 1984.
Alisisitiza kuwa serikali inatambua kazi nzuri na mchango mkubwa wa
Sokoine katika taifa na itaendelea kuenzi na kushirikiana na familia
katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya afya. vijiji
120 vya maeneo husika.
0 Maoni:
Post a Comment