Majaliwa acharuka

Majaliwa acharuka

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi sita ya kujitathimini mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi zake wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, kama yanafanya kazi kwa misingi ya sheria na maadili.
Baadaye, yatahakikiwa na kama yatabainika yanachochea migogoro, yatafutwa.
Pia, Majaliwa amezicharukia NGOs nyingine zinazoitangaza vibaya Tanzania kimataifa kwa kupiga picha za kudhalilisha watoto wakiwa wanatembea kwenye mawe huku wamevaa kandambili kubwa, kuonesha nchi ni masikini. Ametaka NGOs hizo kuondoka nchini, la sivyo serikali itazishughulikia.
“Hizi NGOs zingine si muondoke, nendeni kwingine mkafanye kazi. Halafu nyie mnaotuma picha za kudhalilisha watoto wakiwa wamevaa kandambili kubwa, kudai nchi za nje eti Tanzania ni masikini, tutawashughulikia,” alisema Majaliwa alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro jana.
Aidha alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atakuja wilayani hapo kukagua kazi walizozifanya, wanazozifanya na miradi wanaosaidia jamii.
Majaliwa aliwaambia watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wakurugenzi wa mashirika yasiyo ya serikali, yanayofanya shughuli zake wilayani hapo, kuwa serikali haitaki mashirika chochezi wa migogoro na itayafuta.
Alisema serikali haitasita kuyafuta mashirika yanayofanya kazi wilayani humo, ambayo yapo kwa nia ya uchochezi na kuacha kufanya kazi katika malengo yaliyokusudiwa.
Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo, ina mashirika yasiyo ya serikali 30 ambayo yamesajiliwa, lakini yanayofanya kazi ni 19 tu.
Alisisitiza kuwa haiwezekani serikali isajili mashirika hayo, lakini utendaji kazi wake uwe hafifu.
Alisema ukifuatilia, mashirika hayo utagundua kuwa yanapokea fedha nyingi, lakini hakuna cha maana wanachokifanya kwa wananchi. Alisema serikali ina taarifa ya NGOs hizo zinazopewa fedha na wafadhili.
“Najua taarifa zenu mnapokea kiasi gani cha fedha na mnazifanyia nini, lakini namleta Mkaguzi wa serikali ili akague mnatumiaje fedha zenu, nawapa miezi sita tu halafu ukaguzi utaanza, maana kuna mashirika mengi lakini kazi mnazofanya hazionekani,” alisema Majaliwa.
Alisema baadhi ya mashirika, yana akaunti nchi jirani ya Kenya na mengine kama PWC anapewa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka na shirika la UCRT linapokea Sh bilioni 1.5 kwa mwaka, lakini hajui yanafanya nini.
“Nina taarifa zenu mnapata hela nyingi, lakini mnahudumia vipi jamii hakuna, sasa ngojeni ukaguzi ufanyike halafu nitachukua maamuzi maana kila siku Loliondo kuna nini hapa mnasajiliwa halafu hakuna cha maana,” alisema.
“Kuna nini Loliondo, kwani kila mara Loliondo nina taarifa za kila NGOs zinazofanya kazi hapa, najua mnachokifanya, sasa nawaambia serikali haitawafumbia macho kuona hiki ninachokifanya hapa na ikigundulika mnafanya kinyume na matakwa ya usajili tutazifuta”.
Alisema serikali itazifuta NGOs zote, ambazo zitabainika ni kiini cha migogoro Loliondo. Alitoa hadhari kwa kampuni zinazofanya kazi zake bila usajili, kuwa zikigundulika, zitachukuliwa hatua.
Aliwageukia watumishi wa umma na kuwatahadharisha wale wanaotoa taarifa za migogoro ya ndani kwa wahusika wa NGOs na kisha kuzituma nje ya nchi kwenye mitandao ya kijamii na barua pepe.
Alisema kuwa nao watashugulikiwa, kwa kuwa wanapaswa kuwa majibu ya migogoro na si wasambazaji wa habari mbaya za nchi.
Alisisitiza watekeleze kikamilifu kauli ya ‘Hapa Kazi Tu’ ; na si kutumia NGOs kwa ajili ya kudai kuwasaidia wananchi, huku wakijua kuwa wananchi hawanufaiki na fedha hizo wanazopewa na wafadhili Awali akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Majaliwa alitoa tahadhari kwa madiwani kuacha kushirikiana na watu wa Uhasibu wanaotoa hela kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema baadhi ya madiwani, wanakwamisha miradi ya maendeleo kwa kula fedha kwa sababu ya ukaribu walionao.
Akizungumzia nidhamu ya fedha, Majaliwa alisisitiza kila mtumishi lazima afanye kazi kwa bidii, ikiwemo kutoa huduma bila kuwabagua wananchi kwa itikadi zao za vyama.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment