Wachungaji, waumini wakesha kufukuza mapepo

WACHUNGAJI na waumini wa Kanisa la Efatha walikesha usiku kucha wakisali kuwafukuza pepo walioikumba Shule ya Msingi Kabwe mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa na kubughudhi wanafunzi wa kike pekee shuleni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabwe, Richard Madeni amesema, wasichana wanaosoma darasa la tano na sita wamekuwa wakikumbwa kila mara na 'pepo' shuleni tangu mwaka jana.
Madeni amesema Februari 2018, Mchungaji wa Kanisala la Efatha baada ya kuona tatizo linazidi aliomba Serikali ya Kijiji imruhusu afanye maombi maalumu ili kuwafukuza pepo hao shuleni hapo.
Kwa mujibu wa Madeni, baada ya kubaini licha ya maombezi ya kanisa hilo wanafunzi waliokuwa wakisumbuliwa na 'pepo ' waliongezeka hadi 20, Serikali ya kijiji ilimruhusu mlinzi wa shule hiyo ambaye ni mganga wa kienyeji kutambika shuleni usiku kwa ujira wa Sh 35,000 zilizolipwa na Serikali ya Kijiji.
Amesema mganga huyo alishindwa kulimaliza tatizo hilo kwani wasichana waliendelea kuteseka na jana walimu wa shule hiyo na Diwani wa Kata ya Kabwe, Asante Lubisha walikutana na wazee maarufu kijijini na waganga wa kienyeji kujadili.
"Wazee maarufu na waganga wa kienyeji wamesema tuwape siku mbili ili wajadiliane na kuona la kufanya kuhusu tatizo hilo. Wameafiki kufanya matambiko usiku shuleni hapo lakini tumewaeleza kuwa hatutawalipa ujira wao kwanza hadi tutakapoona matokeo," alisema.
Amesema, waganga wa kienyeji watakaofanya matambiko shuleni hapo usiku ni wale wenye leseni halali za tiba mbadala na sio vinginevyo. "Kesho (leo) watatoa jibu la uhakika na kiasi cha ujira wa kazi watakayoifanya maana wanaweza kuungana na kuwa watano hadi sita, " alisisitiza.
Makamu Mkuu wa Shule ya Msingi Kabwe , Lupa Godwin alikiri tatizo hilo lipo tangu Novemba mwaka jana na limezidi Februari mwaka huu ambapo wanafunzi wa kike 20 wenye miaka tisa hadi 13 wanasumbuliwa na 'pepo hao ' .
"Awali tulikuwa tukiwapeleka zahanati ambapo baadhi yao walibainika kusumbuliwa na malaria lakini hata wakitibiwa wanakumbwa tena na mapepo hivyo siku hizi hatuwapeleki tena zahanati bali tunawaita wazazi wao wanakuja kuwachukua ..... kuhusu mkakati tuliyojipangia kukabiliana na tatizo hili wasiliana na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji (Madeni), " alisisitiza Godwin. Diwani wa Viti Maalumu, Christina Simbakavu alikiri tatizo hilo limedumu muda mrefu na sasa limekuwa kero kwa wazazi, walimu na wakazi.
Mwenyekiti wa Kitongoji namba tatu Kijiji cha Kabwe Asili, Evelina Kazimoto alisema yeye anawafahamu wanafunzi wa kike 10 ambao wazazi wao wamekuwa wakiwapelekea kwenye nyumba za ibada kwa maombezi huku wengine wakiwakimbiza kwa waganga wa kienyeji.
Akizungumza kwa simu, Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Dk Emanuel Mtika alisema shule hiyo ni ya kutwa na wasichana wanaoumwa ni wenye umri chini ya miaka 16 na wachungaji wanafanya maombi bila mafanikio hivyo kuna uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa malaria.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment