Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga mkoani
Rukwa, imewahukumu watu wawili wakazi wa kijiji cha Kaengesa wilayani
Sumbawanga mkoani hapa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia
ya kumbaka mwanamke mmoja na kumsababishia kifo.
Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki
iliyopita na Jaji wa Mahakama hiyo, Dk. Adamu Mambi baada ya kuridhishwa
na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka uliokuwa
na mashahidi wanne.
Waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa
kunyongwa ni Maurus Semwanza na Edward Chikwema ambao walimbaka Magreth
Lazaro kisha kumuingizia kitu chenye ncha kali katika sehemu za siri
hadi utumbo kutoka nje.
Katika shauri hilo ambalo upande wa
mashitaka waliongozwa na mawakili Njoloyota Mwashubila na Safi Kashindi,
huku mshitakiwa akitetewa na Wakili Peter Kamyalile,Ilidaiwa mahakamani
hapo kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Juni 10 mwaka 2012 katika
kijiji cha Kaengesa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ilidaiwa kuwa siku ya tukio majira ya
saa 4 usiku mwanamke huyo akiwa katika moja na baa za pombe ya
kienyeji,alitoka nje kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo ndipo
washitakiwa hao walipomvamia na kumziba mdomoni na matambala kisha
kumpeleka kichakani ambako walimbaka kisha kumuingizia kitu chenye ncha
kali ukeni na kumsababishia utumbo kutoka nje.
Ilielezwa kuwa baada ya kumfanyia
ukatili huo walitokomea kusikojulikana, ndipo mwanamke huyo alipookolewa
na wasamaria wema ambao walimpeleka katika Zahanati ya Kaengesa baadae
hospitali ya mkoa ambako alifariki dunia kutokana na kutokwa na damu
nyingi katika sehemu zake za siri.
Ilidaiwa na mawakili wa serikali kwamba
mtuhumiwa kabla ya kufariki aliwatambua wabakaji hao kwa majina hivyo
polisi walifanikiwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Awali kabla kutolewa kwa hukumu hiyo,
Wakili wa Serikali Mwashubila aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili
iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Akitoa hukumu Jaji Dk. Mambi alisema
watuhumiwa wamekutwa na hatia hivyo kwa mujibu wa kifungu 196 sura 16
cha Sheria ya makosa ya jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwa 2002
washtakiwa wanahukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa.
0 Maoni:
Post a Comment