UTATA umeibuka baada ya miili ya watu
wawili waliouawa na watu wasiojulikana kukutwa katika nyumba ya kulala
wageni mjini Tanga ikiwa haina nguo na imefungwa kamba za miguu na
mikononi.
Katika tukio hilo ambalo limethibitishwa
na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedicto Wakulyamba miili ya watu
wawili, wote wanaume, iligunduliwa jana majira ya saa mbili asubuhi na
mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Bomai Inn iliyopo Kata ya Majengo
jijini Tanga.
Kamanda Wakulyamba aliwaambia waandishi
wa habari jijini Tanga jana kuwa mhudumu wa nyumba hiyo ambaye hakumtaja
kwa jina, alibaini kuwapo kwa miili hiyo alipotaka kufanya usafi ndani
ya chumba hicho.
"Majira ya saa mbili asubuhi wakati
mhudumu alipoingia ndani ya chumba hicho namba 303 kwa ajili ya kufanya
usafi, alikutana na miili ya watu hao wawili wote ni wanaume ikiwa
imelala chini, imefungwa kamba miguuni na mikononi," alisema.
Kamanda huyo alisema miili hiyo ni ya watu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40 ambao hawakutambulika mara moja.
Alisema kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu za
kitabu cha wageni cha nyumba hiyo ya kulala wageni, mtu anayeitwa
Rashid Omari alijiandikisha kutumia chumba hicho siku hiyo.
Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, Omari ni Msafa kwa kabila, mkazi wa Dar es Salaam na ni mfanyabiashara.
Kamanda Wakulyamba alisema miili hiyo
haikuwa na jeraha lolote zaidi ya michubuko ya kawaida na kwamba Jeshi
la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini sababu za mauaji hayo na
waliohusika kuyatekeleza ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Vifo vya watu hao vimezua utata kutokana
na waliouawa kutofahamika kwa wakazi wa eneo hilo, mazingira ya vifo
vyao kuashiria mauaji, wauaji kutojulikana pamoja na kitendo cha uongozi
wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuruhusu wanaume wawili walale chumba
kimoja, kinyume cha taratibu za uendeshaji wa biashara hiyo.
"Watu wawili tena wanaume kuuawa ndani
ya chumba kimoja na kusiwe na hata mtu aliyesikia kurupushani za mauaji
hayo... inatia hofu kubwa na inawezekana kuna mpango maalum wa wauaji
hao," alisema Asha Ramadhan, mmoja wa walioshuhudia tukio hilo la utoaji
miili hiyo.
Hamza Issa, mkazi mwingine wa maeneo
hayo, alisema huenda mauaji hayo yalipangwa na aliyelipia kutumia chumba
hicho kabla ya kukutwa miili ya watu wawili.
Mkazi mwingine wa maeneo hayo, Anthon
Aloys, alisema huenda maiti hizo ziliingizwa ndani ya chumba na
mkodishaji chumba hicho baada ya watu hao kuuawa eneo jingine.
WATU WATATU
Matukio ya wanaume zaidi ya mmoja kuuawa
wakiwa katika chumba kimoja cha nyumba za wageni yalififia kwa muda
lakini si uhalifu ambao ni mgeni.
Machi 21, mwaka jana watu watatu
walikutwa wakiwa wameuawa kwa kunyongwa katika nyumba ya kulala wageni
ya Mexico, mjini Kyela mkoani Mbeya, ikiwa na majeraha ya kuunguzwa kwa
moto.
Mganga mfawidhi wa Hosptali wa Wilaya ya
Kyela, Dk. Francis Mhagama alikaririwa akisema maiti hizo za watu
watatu zilikuwa zimenyongwa pamoja na majeraha ya moto.
Kwa mujibu wa kitabu cha wageni cha nyumba hiyo, majina ya watu hao yalikuwa Hassan Ally, Mariam Hassan na Adam.
Aidha, Agosti mosi, mwaka jana pia watu
wawili walikutwa wamefariki katika nyumba ya wageni ya Kings Rest House
iliyopo Mtaa wa Bumila, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam huku miili
yao ikiwa imeungua moto.
Watu hao waliofariki walikuwa
wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi
walipokuja jijini walifikia hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum
Hamduni alisema mmoja wa waliofariki alijiandikisha kama Lameck
Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.
0 Maoni:
Post a Comment