UWANJA wa ndege wa Kahama uliokuwa ukimilikiwa na Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia kupitia mgodi wa Buzwagi mkoani Shinyanga, umekabidhiwa rasmi kwa serikali. Uwanja huo ambao ulikuwa chini ya mgodi wa Buzwagi, umekabidhiwa jana, ikiwa ni maandalizi ya kampuni hiyo kumaliza shughuli zake za uchimbaji katika mgodi huo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack wakati akizindua safari za ndege za Shirika la Precision Air katika wilaya ya Kahama mkoani humo. Telack alisema, uwanja huo ulikuwa hautumiki mara kwa mara, hivyo wakafanya mazungumzo na wamiliki wake ili serikali iweze kuuchukua na kuendelea kuhudumia Watanznia mbalimbali wa Mkoa wa Shinyanga.
“…Si mara nyingi wanaleta ndege, tukaona kwa nini serikali tusitumie uwanja huu kuwahudumia wananchi wa hapa, lakini pia mwaka huu tutakuwa na uwanja wa ndege wa Shinyanga hivyo haya ni maandalizi,” alisema Telack.
Akizungumzia safari za shirika hilo, Telack alisema, kwa sasa itakuwa ni nafuu kwa wakazi wa Shinyanga na wilaya zake, kwani zamani walikuwa wakilazimika kutumia saa mbili au zaidi kwenda Mwanza kupanda ndege.
Aliongeza pia hatua hiyo itasaidia kuongeza, wawekezaji wengi zaidi kwani ili wawekezaji waweze kufanya kazi zao vizuri wanahitaji usafiri wa uhakika na hasa wa anga. “Sasa hivi kutakuwa hakuna tena usumbufu wa kwenda Mwanza, lakini hii ni fursa kwenda, wafanyabiashara na wawekezaji wanaweza kuja Shinyanga asubuhi wakafanya shughuli zao na kisha jioni wakirudi Dar es Salaam, na kwa vile Shinyanga tunalima mpunga, wanaweza kuja kununua,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu alisema kwa sasa uwanja huo, utaweza kuhudumia wakazi wa wilaya za mkoa huo pamoja na wilaya za jirani na kwamba Tanzania inapoelekea katika uchumi wa viwanda inahitaji kuwa na usafiri wa uhakika.
Kwa upande wake, Meneja Uratibu na Uhusiano wa Precision, Hillary Mremi alisema, lengo la kuanzisha safari hiyo ni kufungua nchi na kuwahudumia Watanzania wengiu zaidi. “Tunaendelea kuifungua Tanzania, tunalenga kufikia maeneo mbalimbali nchini ili kuleta maendeleo kwa Taifa letu,” alisema Mremi. Alisema shirika hilo linaendelea kujidhatiti ili kuhakikisha mikoa mingi inafikika kwa urahisi.
0 Maoni:
Post a Comment