Mtuhumiwa
wa mauaji ya watoto wawili, Moureen David (6) na Ikram Salum (3),
amekiri kuwateka watoto hao, kuwaua na kuwatumbukiza ndani ya shimo la
maji taka.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, mtuhumiwa
Samson Peter (18), alipomaliza kuwateka watoto hao na wengine kuwaachia,
alikimbilia mkoani Geita ambako alikamatwa Septemba 2 mwaka huu kisha
kuletwa jijini Arusha, Septemba 4, mwaka huu.
Kamanda
Mkumbo alisema baada ya mahojiano, Peter alikiri kuwateka watoto hao na
wengine kuwaachia kisha kukiri kuwaua Ikram na Moureen na kuwatumbukiza
ndani ya shimo la maji taka lililopo katika nyumba ambayo haishi mtu na
haijamalizwa kujengwa iliyopo eneo la Mtaa wa Olkerian katika Kata ya
Olasiti. Alisema askari baada ya kufika eneo hilo huku wakiwa na
mtuhumiwa huyo, waliikuta miili ya watoto hao ikiwa inaelea juu ya maji
yaliyopo ndani ya shimo hilo.
Aliongeza
kuwa licha ya matukio hayo mawili, mtuhumiwa huyo Agosti 28, mwaka huu
saa 11:45 jioni eneo la Kwamrombo, aliwateka watoto wawili ambao ni Ayub
Fredy mwenye umri wa miaka mitatu na miezi minne na Bakari Suleiman
mwenye umri wa miaka mitatu na miezi miwili na baada ya juhudi za Jeshi
la Polisi na wananchi, walifanikiwa kuwapata watoto hao siku hiyo hiyo
muda wa saa 2:00 usiku.
Alisema
polisi kwa sasa wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo ambaye anatarajia
kufikishwa mahakamani muda wowote mara upelelezi utakapokamilika.
Awali,
Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Daudi Safari alisema wazazi wa watoto
hao wanasubiri uchunguzi wa kitaalamu wa madaktari ili waruhusiwe
kuchukua miili hiyo na kwenda kuizika kwani imeharibika vibaya na
kusisitiza kuwa mtoto Ikram atazikwa muda wowote leo baada ya kukamilika
kwa taratibu hizo za kiuchunguzi.
0 Maoni:
Post a Comment