Taharuki Kenya huku matokeo ya uchaguzi wa urais yakisubiriwa kwa hamu

Hali ya taharuki imetanda nchini Kenya huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo (IEBC) ikitazamiwa kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais wakati wowote tokeo sasa hii leo.

Duru za habari zinasema watu wasiopungua wanane wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika machafuko ya baada ya uchaguzi nchini humo hadi sasa, taifa ambalo lilishuhudia mauaji ya watu 1,200 katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

IEBC imesema matokeo itakayoyatangaza hii leo yatakuwa ni kwa mujibu wa sheria na maamuzi ya wananchi na wala hayataegemea mashinikizo ya shakhsia au mrengo fulani wa kisiasa.
Hapo jana mrengo wa upinzani wa NASA uliitaka IEBC imtangaze mgombea wa muungano huo Raila Odinga kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo siku ya Jumanne.
Raila Odinga (Kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta
Viongozi wa NASA wanasema vyanzo vyao vya siri ndani ya IEBC vimewapa ithibati kuwa Odinga amepata kura zaidi ya milioni nane huku Rais Uhuru Kenyatta aliyewania kiti hicho kwa muhula wa pili kupitia Chama cha Jubilee akipata kura milioni saba na laki saba. 

Hii ni katika hali ambayo, kufikia sasa matokeo ya IEBC yanaonesha kuwa, Kenyatta anaongoza kwa kura zaidi ya milioni 8, ambazo ni sawa na asilimia 53.89 ya kura zilizohesabiwa huku mpinzani wake mkuu, Raila Odinga akiwa na kura zaidi ya milioni sita na laki saba ambazo ni sawa na asilimia 44.47 ya kura.

Aghalabu ya timu za waangalizi wa uchaguzi huo zikiwemo Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Kieneo ya IGAD zinasema kuwa, uchaguzi huo ulikuwa huru, wa haki na wazi.

Viongozi wa NASA walisema kuwa, watatoa mwelekeo na msimamo wao hii leo baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo yake ya uchaguzi wa rais.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment