Aliyasema hayo kwa hisia kali na kuonesha masikitiko yake dhidi ya unyanyasaji wa mwili wa marehemu kaka yake uliofanywa katika Hospitali ya Sinza Palestina ambayo ni ya Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alisema mwili wa marehemu huyo, ulitupwa kwenye gari kama mzoga ulipokuwa ukipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala wilayani Kinondoni. Simbachawene alisema hayo kwenye kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya mjini hapa.
Aliwataka viongozi hao, kuchukua hatua kali ikiwemo kuwafukuza kazi watumishi wanaonyanyasa wagonjwa ili kukomesha tabia hiyo, ambayo inachafua sekta ya afya nchini. Pia alitaka Hospitali ya Sinza Palestina, iangaliwe kutokana na kukithiri kunyanyasa wagonjwa na hata miili ya watu waliofariki pindi wanapotaka kuchukuliwa na ndugu zao.
Alisema baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo, wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa ndugu wa marehemu, hali ambayo imekuwa ikizidisha uchungu mara mbili. Alisema ni jambo lisilokubalika kuona baadhi ya watumishi wachache, wanaendelea kuichafua sekta ya afya bila kuchukuliwa hatua.
“Haya mambo uhadithiwe tu, lakini usikutane nayo, hivi karibuni nilifiwa na kaka binamu katika Hospitali ya Sinza Palestina, kumbe alikuwa na tatizo la kifua kikuu ambalo halikugundulika mapema,” alisema.
Alisema mkewe (mke wa waziri Simbachawene) alikuwa hospitalini hapo ili kushughulikia mwili wa marehemu, ukipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala.
“Kuanzia saa nane mpaka saa 12 jioni watu wanasubiri tu gari huku wakiambulia matusi na kejeli kutoka kwa watumishi wa pale, wakiwemo wauguzi,” alisema. Alisema jambo hilo lilimuumiza sana, kwani inaonesha dhahiri wananchi wanavyonyanyasika kwenye hospitali za umma.
“Nikaanza kujilaumu, je, sikutimiza wajibu wangu, nikasema kwa yale wanayofanya watakutana na Mungu wao,” alisema. Alisema wakati mke wake akihangaika hospitalini hapo huku akishambuliwa kwa maneno makali, ndipo akatokea daktari ambaye alikuwa akimfahamu ambaye aliingilia kati suala hilo.
“Baadaye maiti ikatolewa na kuwekwa kwenye gari zile za Kirikuu (Suzuki Carry), maiti ikatupwa kwenye gari, inatia uchungu sana,” alisema waziri huyo. Alisema kwenye sekta ya afya, kuna watumishi wabaya na wema wapo pia.
Alisema mambo kama hayo, yamekuwa yakichafua sekta ya afya nchini, kwani vitendo hivyo vinatokea mara nyingi lakini hakuna anayechukua hatua. “Wabaya wapo na kuna wanaofanya vizuri, sasa tunataka kuona mashitaka yanapelekwa kwenye ngazi zinazohusika na waganga wakuu wa mikoa na wilaya,” alisema.
Alisema sasa mashitaka kama hayo, yamekuwa yakipelekwa na wanasiasa au viongozi kutokana na waganga wakuu kutochukua hatua. “Ninyi si viongozi wazuri, ndio maana hamchukui hatua na matukio kama haya yanazidi kuendelea.
Hakikisheni mnachukua hatua wasomi wako wengi, wakitolewa tutaajiri wengine,” alisema. Alisema kuna watumishi wanaofahamika kuwa na lugha chafu, kutoa huduma mbovu, lakini wamekuwa wakiweka maslahi mbele, hao ni wa kuangaliwa sana.
0 Maoni:
Post a Comment