Viongozi NEMC wafyekwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January MakambaWaziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba

SERIKALI imevunja Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC), sambamba na kufanya mabadiliko ya uongozi huku watumishi wanne wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema hatua hiyo imetokana na kukithiri kwa malalamiko ya wananchi na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

“Tunapoelekea kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, usimamizi wa mazingira lazima uwe imara na urahisishe na kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa viwanda, miradi mbalimbali na uwekezaji katika sekta zote ili kwenda kwa kasi na weledi unaotakiwa,” alieleza January.Aliongeza: “Utendaji wa NEMC umekuwa ukilegalega sana na umekuwa hauridhishi jambo ambalo limeibua malalamiko mengi kwa wawekezaji wa ndani na nje.”

“Tumejitahidi kurekebisha hali hii na kumejitokeza nafuu, lakini bado hali haijafikia pale nilipotarajia. Nimefuatilia kwa karibu na kugundua kuwa matatizo mengi yanasababishwa hasa na usimamizi usio imara wa bodi na pia watendaji wakuu wa NEMC.

Nimeamua kutengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye niteue wajumbe wapya ambao wataenda na kasi na ari tunayoihitaji sasa katika kuelekea uchumi wa viwanda.” 

Alisema Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni ya Rais, ataendelea kuwepo hadi hapo atakapoteuliwa mwingine. Alisema amemteua Dk Elikana Kalumanga, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC hadi hapo rais atakapofanya uteuzi kwa nafasi hiyo. Kalumunga ni Mhadhiri katika Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema ili kuboresha utendaji wa NEMC, amefanya mabadiliko ya baadhi ya wakurugenzi na wakuu wa kanda, kwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa NEMC, Charles Wangwe kumrejesha Wizara ya Fedha na Mipango atakapopangiwa kazi kulingana na mahitaji ya serikali.


Nafasi hiyo itakaimiwa na Adam Minja kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais. Aliwataja wakuu wa kanda waliobadilishwa ni Jafari Chimgege aliyekuwa Kanda ya Mashariki anakwenda Kanda ya Kati- Dodoma, Goodlove Mwamsojo aliyekuwa Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu –Mbeya atakuwa Mkuu wa Kanda ya Mashariki- Dar es Salaam.

Pia Dk Ruth Rugwisha aliyekuwa Mkuu wa Kurugenzi ya Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Sheria, sasa atakuwa Mkuu wa Kanda ya Ziwa-Mwanza, Dk Vedastus Makota aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma atakuwa Mkuu wa Kanda ya Kusini- Mtwara na Joseph Kombe aliyekuwa Mkuu wa Kurugenzi ya Utafiti na Mipango wa NEMC anakwenda kuwa Mkuu wa Kanda ya Kaskazini- Arusha.

Mabadiliko hapo pia yamemgusa Dk Menard Jangu aliyekuwa Arusha ambaye anapanda na anarudishwa Makao Makuu ya NEMC kuwa Kaimu Mkuu wa Kurugenzi ya Utafiti na Mipango huku Jamal Baruti aliyekuwa Mkuu wa Kanda ya Ziwa anarudi Makao Makuu na Lewis Nzari aliyekuwa Mkuu wa Kanda ya Kusini -Mtwara, sasa anakuwa Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini- Mbeya. Pia Risper Koyi wa Ofisi ya Makamu wa Rais ameteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria NEMC kuchukua nafasi ya Jandwa anayehamishiwa Kanda ya Kati-Dodoma.

Pia Dk Yohana Mtoni ambaye ni Ofisa Mazingira Mkuu NEMC anakuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Sheria kumbadili Rugwisha ambaye anakwenda Kanda ya Ziwa- Mwanza, na Carlos Mbuta aliyekuwa Ofisa Mawasiliano Mkuu wa NEMC ameteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa NEMC. Aidha, January alisema wamewasimamisha kazi watumishi watumishi wanne ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za utendaji wao; ambao ni mwanasheria Manchare Heche, Deus Katwale, Andrew Kalua na Benjamin Dotto.

Alifafanua kuwa malalamiko yaliyokithiri NEMC ni ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), tuhuma za rushwa katika mchakato wa ukaguzi na utengeneza vyeti ambavyo havijafuata mchakato.

Alisema pia kumekuwapo na malalamiko ya kutokuwa na lugha nzuri kwa wateja na kuwatisha ili watoe chochote, kutumia kampuni binafsi ya watumishi wa NEMC kufanya kazi za ukaguzi kwa kisingizio cha kutokuwa na watumishi wa kutosha na kuwaelekeza wawekezaji kufanya kazi na kampuni inayomilikiwa au yenye ubia na watumishi hao.

Katika hatua nyingine, January ameagiza ruksa ya ujenzi itolewe ndani ya siku tatu za kazi kwa miradi yote inayohusu ujenzi wa viwanda, baada ya mwekezaji kuwasilisha taarifa hitaji la ujenzi wa kiwanda kwa NEMC. Alisema kuanzia sasa miradi itakayopelekwa NEMC kuombewa cheti cha EIA ni ile ambayo tayari imefanyiwa kazi na washauri elekezi. “Hapatakuwepo na haja ya kusajili mradi NEMC kwanza.

Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment