Wakati
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu
Lissu, akiwa bado anakabiliwa na kesi kadhaa za uchochezi, amefytuka
tena na kutoa maneno mazito juu ya viongozi wa Serikali, huku akisema
kwa mujibu wa sheria za nchi, anaweza kukamatwa, lakini si kufungwa.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana,
Lissu pia alisema amepata taarifa kutoka kwa mmoja wa askari polisi kuwa
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, atafikishwa mahakamani wakati
wowote kutokana na kauli alizozitoa juu ya masheikh wa Uamsho. Hata
hivyo, Mpekuzi haikuweza kujiridhisha juu ya usahihi wake.
Tundu
Lissu ambaye baadhi ya kauli zake haziandikiki kwa sababu za
kimaadili, alisema pia watu ambao wanataka rais aongezewe muda wa
kuongoza baada ya miaka 10 ya kikatiba, wabaki na kile alichokiita ni
ujinga wao.
“Kuna
watu wanaongea habari za kuongeza muda wa urais, tuwaambie tu huo
wanaoleta ni ujinga, hivyo kaeni na ujinga wenu nyumbani kwenu,” alisema Lissu.
Akizungumzia
taarifa za Lowassa kufikishwa mahakamani, alisema amezipata kutoka kwa
mmoja wa maofisa wa ngazi za juu ndani ya Jeshi la Polisi.
Lissu
alisema kuwa aliwasiliana na ofisa huyo jana asubuhi na kumtaka
ajiandae kwa kesi hiyo ambayo ipo mbioni kupelekwa mahakamani.
“Nina
taarifa nimeambiwa leo na lipolisi likubwa kabisa, maana hata wao
hawafurahi sana, nimeambiwa jiandaeni mheshimiwa Lowassa atafikishwa
mahakamani na kushtakiwa kwa uchochezi kwa sababu ya kuzungumzia uonevu
wanaofanyiwa masheikh wa Uamsho,” alisema Lissu.
Alipoulizwa
endapo kinga za kushtakiwa kwa viongozi, inawahusu pia mawaziri wakuu
wastaafu, alisema kinga inamuhusu rais aliyepo madarakani pekee na mambo
aliyofanya wakati akiwa Ikulu.
Hata hivyo, alisema kinga hiyo kwa marais, imechangia viongozi wengi wakiwa madarakani kufanya mambo mabaya.
“Kuna
marais ambao ni wahalifu wakiwa marais, tunatakiwa tuwe na usawa ndani
ya sheria, ikiwa muhalifu ukiwa Ikulu tukushughulikie au ukitoka
tukushughulikie,” alisema Lissu huku akitolea mfano kwa Rais wa Brazil, Lula Da Silva.
Alisema Da Silva, sasa amehukumiwa kifungo cha miaka tisa baada ya kutoka madarakani kwa makosa ambayo aliyayafanya akiwa rais.
Alisisitiza kiongozi anapaswa kuwa na kinga kwa sababu ni msafi na si sababu ya uongozi wake.
Lowassa
ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifika kwa mara ya kwanza
polisi Juni 27, mwaka huu kwa wito wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (DCI) na kuhojiwa kwa saa nne.
Aliripoti tena Makao Makuu ya Polisi Juni 29, Julai 13 na ametakiwa kuripoti Julai 20.
0 Maoni:
Post a Comment