ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema uteuzi aliyoufanya Rais John Magufuli kwa kiongozi wa Chama cha ATC Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ni sahihi.
Sadiki aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, Rais hajakosea kumteua Mghwira kuwa kiongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwani mwana mama huyo ni mchapakazi, mzalendo na asiye na ubaguzi, na uongozi unahitaji mtu wa aina hiyo. “Nilimfuatilia Mghwira katika kampeni zake akiomba urais, ni mwanamke mtulivu, mwenye mtazamo wa maendeleo na mkoa huu wa Kilimanjaro unataka mtu atayetazama watu kwa maendeleo na si kwa vyama,” alisema Sadiki.
Alisema kuna maeneo matano ambayo angependa mteuliwa huyo ayape kipaumbele ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji. Alisema kama mazingira yataharibiwa zaidi ndani ya miaka 10 mkoa utakuwa jangwa na na kukumbwa na baa la njaa. Katika eneo hilo, alitaka Mghwira ashirikiane na taasisi na viongozi wengine kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Eneo jingine ni uvushwaji wa bidhaa za magendo kutoka Tanzania kwenda Kenya. Alisema mkoa unakosa mapato mengi kutokana na mbinu za ujanja za wafanyabiashara wasio waaminifu. Alimtaka kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujipanga vyema kudhibiti hilo. Dawa za kulevya Alisema kuwa zimekuwa zikiathiri maendeleo ya mkoa.
Akatolea mfano Same ambako mirungi inalimwa sana na kumtaka alishughulikie huku akiwataka wananchi kumpa ushirikiano kuwafichua wanaofanya biashara hiyo haramu. Mimba mashuleni Alieleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana hadi Februari mwaka huu wamepatikana wanafunzi 38 wenye mimba kwenye wilaya ya Same pekee. Amesema kwa kuwa mama Mghwira ni mwanamke, anayo nafasi ya kuzungumza kwa ndani na mabinti na wanawake wasikatishe masomo.
Siasa Alisema kuwa mtu akiwa nje ya mkoa wa Kilimanjaro anaweza akawa na mtazamo hasi wa siasa za Kilimanjaro, ila hilo si tishio kwani anaamini kuwa kiongozi kwenye mkoa huo anashirikiana na wananchi na maendeleo yanapatika. ACT inasemaje Wakati Sadiki akiwa alishaachia ngazi hiyo na Rais tayari ameshamtangazia uteuzi wa nafasi hiyo mama Mghwira, Chama cha ACT Wazalendo kimesema hatua ya Rais Magufuli kuwateua viongozi wa chama hicho kushika nyadhifa mbalimbali katika utawala wake ni kuonesha kuwa chama hicho kina watu wenye uwezo wa kufanya kazi nzuri na upinzani wana uwezo vile vile.
Hata hivyo, kimesema uteuzi wa Rais kwa Mwenyekiti wa chama hicho Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ni pigo kwa chama hicho kwani bado kilikuwa kinamhitaji. Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu alisema, “Kwetu tumepoteza hatuwezi kusema tunafurahia uteuzi huu kwa sababu huwezi kumpa mtu keki yako unayoipenda na wewe ukabaki na keki,” alisema Ado.
0 Maoni:
Post a Comment