Magufuli: IGP fumua jeshi la polisi, komesha uhalifu

Rais John Magufuli akifungua Kikao cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi na Makamanda wa Mikoa na Vikosi katika Bwalo la Maafisa wa Polisi la Oysterbay jijini Dar es Salaam jana. Picha ya chini ni Maafisa hao wakimsikiliza. (Picha na Ikulu). 
RAIS John Magufuli amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro (pichani) kupangua na kujipanga vizuri na safu yake ya makamanda, viongozi wakuu wa vikosi na maofisa mbalimbali ili kukabiliana na uhalifu na kuondoa dosari zote za utendaji zinazohusiana na ufanisi na heshima ya jeshi hilo.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na makamanda wakuu kutoka makao makuu ya polisi, makamanda wa mikoa na vikosi vya Tanzania Bara na Zanzibar na viongozi wote wakuu wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Alikutana nao katika Bwalo la Maofisa Wakuu wa Polisi lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam. “Ni lazima ufanye mabadiliko makubwa, nataka kuona Jeshi la Polisi linakuwa Jeshi la Polisi, Wewe IGP Sirro na Makamanda wenzako hakikisheni mnakomesha uhalifu, komesheni mauaji dhidi ya raia, ujambazi na dawa za kulevya,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli aliwataka makamanda, maofisa na askari wa jeshi hilo, kujiepusha na rushwa, dawa za kulevya, kutumiwa na watu kwa maslahi binafsi, kuingia mikataba isiyo na maslahi kwa Jeshi na Taifa, ubadhirifu na kuacha upendeleo katika utoaji wa ajira na vyeo.

Rais alilitaka pia jeshi la polisi nchini kutumia weledi wake kwa kiwango cha juu katika kutekeleza jukumu lake la kulinda raia na mali zao, hasa kukomesha vitendo vya uhalifu.

Alilipongeza jeshi hilo kwa juhudi zake za kukabiliana na uhalifu, lakini alilitaka liongeze juhudi hizo hususani kukabiliana na matukio ya ujambazi na mauaji ya raia, dawa za kulevya na kuendesha operesheni zenye tija katika mikoa yote.

Rais Magufuli aliwataka makamanda, maofisa na askari polisi wote wampe ushirikiano wa kutosha IGP Sirro, ambaye hivi karibuni amemteua kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment