Askari
wa Jeshi la Polisi, Kituo cha Kigamboni wanadaiwa kumuua kwa kumpiga
risasi tumboni, mwanafunzi wa Chuo cha cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo
Boniventure Kimali (25), wakimtuhumu kuwa ni jambazi.
Tukio
hilo la kusikitisha lilitokea saa 3:30 usiku wa kuamkia juzi huko
Kigamboni Vijibweni, nyumbani kwa kaka wa marehemu aitwaye, Naftan
Barampami ambaye alikuwa akiishi naye.
Akisimulia
jinsi ilivyokuwa, Barampami alisema usiku huo wakiwa bado wapo nje ya
nyumba yao huku kila mmoja akiendelea na shughuli zake ndogo ndogo na
wengine wakiwa wamejipumzisha, ghafla walishangaa kusikia milio ya
risasi zilizopigwa mfululizo.
“Tulishtuka,
milio hiyo ilitokea upande wa uwanjani ambapo ni jirani na nyumbani
kwetu, tuliogopa kila mtu ilibidi atafute namna ya kujiokoa, tulikimbia,
mimi nilikimbilia ndani, Boni alikimbia kuelekea nyuma ya nyumba yetu,” alisema.
Alisema akiwa ndani ya nyumba yake alisikia mtu akilia huku akiwasihi watu waliokuwa wamemzingira wasimuue.
“Ikabidi
nisogee jirani zaidi na dirisha, nikakaa kwa utulivu na kuangalia nje
kupitia dirishani kilichokuwa kikiendelea, ghafla nilimsikia Boni akilia
kwa uchungu huku akiugulia maumivu, kumbe walikuwa tayari wamempiga
risasi,” alisema.
Alisema
askari wote walikuwa wamevaa kiraia, marehemu alikuwa akiendelea
kuwasihi wasimuue huku akiwasihi wamuwahishe hospitalini kwani alikuwa
akisikia maumivu makali.
“Aliwaomba
wampekele hospitali na watujulishe ndugu zake lakini hawakumsikiliza,
punde alifika mwenzao ambaye alishtuka na kuwaeleza wenzake wamefanya
kosa kwani waliyempiga risasi si jambazi ambaye walikuwa wanamtafuta,” alisema.
Alisema
japo alitamani kutoka nje ili akamsaidie ndugu yake lakini alihofia
maisha yake kwani mmoja wa askari hao alionya asitokee mtu yeyote katika
eneo hilo.
“Niliogopa
mno, ikabidi nibaki pale pale dirishani nikifuatilia, nilihofu iwapo
nisingetii amri hiyo na kutoka nje na mimi wangenipiga risasi,” alisema.
Barampami
alisema akiwa dirishani hapo, alimshuhudia yule askari aliyefika katika
eneo hilo akichukua simu yake na kuwasiliana na wenzake ambao aliwataka
wawahishe gari haraka katika eneo hilo.
“Lilipofika, walimchukua marehemu wakampakiza ndani ya gari hilo na kuondoka naye, wakati huo alikuwa bado anaugulia maumivu,” alisema.
Alisema
baada ya muda kupita eneo hilo lilikuwa shwari akatoka nje na baadhi ya
ndugu zake na kwenda kituo kidogo cha Polisi Vijibweni.
“Pale
tuliuliza kama walikuwa wamemfikisha hapo, askari tuliyemkuta
alituambia walielekea Kituo Kikuu cha Polisi Kigamboni, tukaenda huko,” alisema.
Alisema
walipofika walipokewa na baadhi ya askari waliowakuta ambao waliwaeleza
ndugu yao alikuwa amepelekwa Hospitali ya Vijibweni kwa matibabu.
“Tukaenda
hadi huko lakini daktari mmoja alituambia hawakumpokea na kumuhudumia
kwani hawakuwa na maelezo yaliyojitosheleza, tukarudi Kigamboni lakini
awamu hii hatukupewa ushirikiano kama awali, tulipewa amri tusisogee
katika eneo hilo,” alisema.
Alisema
waliwasiliana na ndugu zao kuwaeleza hali waliyoikuta akiwamo ndugu yao
Daudi Gwelenza ambaye anafanya kazi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI).
“Tuliwataka
wajaribu kupita katika hospitali mbalimbali kumtafuta hasa Muhimbili,
ndipo Gwelenza akaenda pale chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema.
Gwelenza
alisema alipofika hapo alielezwa kuna mwili ambao umefikishwa na askari
wa Kigamboni, aliruhusiwa kuuona ndipo akakuta ni ndugu yake huyo.
“Nilimuangalia
sura nikakuta ni yeye, nikamwangalia tumboni kweli alikuwa amepigwa
risasi eneo la kushoto tumboni, alikuwa na mchanga mwingi wa bahari
inaonesha huenda aliburuzwa, nilisikitika mno sikuweza tena kuendelea
kuangalia tena,” alisema.
Aliongeza “Lakini
nishangaa kwanini katika maelezo yaliyoandikwa juu ya taarifa ya
marehemu hawakuandika kwamba amepigwa risasi, waliandika tu amepigwa na
waliandika hajulikani jina lake, yaani kama vile walimuokota mahali
akiwa ameuwawa.
Katika eneo hilo kulipatikana maganda mawili ya risasi yenye namba 311 (10) na 10 (77).
Msemaji wa familia, Goodluck Kimali ambaye ni kaka wa marehemu, alisema kitendo kilichofanywa na askari hao hakivumiliki.
“Kwa
mujibu wa majirani na mashuhuda wa tukio hili, wanasema angewahishwa
hospitalini asingepoteza maisha, kwanini hawakumuwahisha huko, kwanini
walimpiga risasi tumboni na si mguuni ili asiwakimbie, kwa sababu hakuwa
na silaha yoyote, kwanini walimuua,” alihoji.
Alisema
tangu kutokea kwa tukio hilo hakuna askari yeyote aliyefika nyumbani
hapo kukagua, kujiridhisha juu ya kile walichokuwa wakimtuhumu marehemu.
“Hatujamuona
askari hata mmoja kukagua, kwanini hawajafika kufanya ukaguzi, hii
inamaanisha wanajua walichokifanya, kitendo hiki hakivumiliki, Tanzania
ni nchi ya amani, askari anapaswa kulinda raia na mali zake, lakini
imekuwa kinyume chake,” alisema.
Alisema ingawa wanafuatilia kwa ukaribu suala hilo hata hivyo hawaoni kama kweli watasaidiwa kupata haki ya ndugu yao.
“Kuna
urasimu mwingi nauona, tunaomba watupe mwili wa ndugu yetu
tukampumzishe, maana hata tukisusa na kuwaachia hawawezi kurejesha uhai
wake, lakini vitendo hivi vikomeshwe, sisi tunavumilia lakini ipo siku
raia watachoka,” alisisitiza.
Alisema
watakapokabidhiwa mwili huo, wanatarajia kuusafirisha wakati wowote
hadi kijijini kwao Mwayeye, Wilaya ya Buligwe mkoani Kigoma kwa ajili ya
maziko.
Mkurugenzi
wa Mafunzo na Utafiti wa Chuo cha Mbegani, Ambaksye Simtoe alisema
tukio hilo limewashtua kwani marehemu alikuwa kijana mtulivu, msikivu na
mpole.
“Alikuwa
anasoma kozi ya Uchakataji Samaki, Ubora na Masoko, ngazi ya Diploma,
mwaka wa tatu, Juni, mwaka huu angehitimu masomo yake.
“Alikuwa
yupo field (mafunzo kwa vitendo) katika Soko la Kimataifa la Samaki
Feri, tumesikitika mno, kifo chake kimekuwa cha ghafla hatukutarajia
kama ipo siku haya yatatokea,” alisema.
0 Maoni:
Post a Comment