Bunge lawasamehe Mbowe, Mdee, Makonda

Image result for bunge job ndugai
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wabunge Halima Mdee na Esther Bulaya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Elexander Mnyeti, wamenusurika kukumbwa na hukumu ya Pilato baada ya Bunge kuwasamehe.
Wabunge hao na viongozi wa Serikali wamesamehewa makosa yao tofauti kudharau Kiti cha Spika na kulidharau Bunge, baada ya kusimama mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na kuomba radhi makosa waliyotenda.
Katika msamaha huo, wakati Mbunge wa Bunda Vijijini, Bulaya (Chadema) amesamehewa kwa kuandikiwa barua ya karipio, Mbunge wa Kawe, Mdee (Chadema) aliyeadhibiwa na Kamati kwa kutakiwa kutohudhuria bunge la Bajeti, wabunge wakamwombea msamaha badala yake akapewa adhabu ya kuhakikisha hatendi kosa, akitenda ataadhibiwa na kiti cha Spika bila hata kulepekwa mbele ya Kamati.
Mbowe, Makonda na Mnyeti walisamehewa na Bunge bila masharti yoyote kutokana na kuomba radhi kwa makosa waliyofanya kwa nyakati tofauti. Mnadhimu wa Bunge, Jenista Mhagama alisema adhabu ya Mdee aliyopewa na Kamati, alisimama bungeni na kuomba bunge libadilishe adhabu yake badala ya kukaa nje ya Bunge la Bajeti kwa miezi miwili tangu jana, asamehewe lakini akifanya kosa lingine basi hataenda mbele ya kamati ya haki atapewa adhabu pale pale na Spika.
“Halima Mdee asemehewe kosa alilofanya, ila tu iwapo atatenda kosa lingine la kudharau kiti cha Spika na kudharua mamlaka ya Bunge kadiri ya kifungu namba 26 (d) ya Kanuni za Bunge sura 296, utekelezaji wa adhabu hiyo utatakiwa uanze mara moja kwa maelekezo ya kiti cha Spika bila kufuata maelekezo ya kamati ya Bunge,” alisema.
Spika alipowahoji wabunge walikubaliana na kubadilishwa kwa adhabu iliyotolewa na kamati na badala yake itumike ya Mnadhimu wa Bunge, ambayo inataka badala yake mbunge atatakiwa kutotenda kosa lingine na akirudia kiti cha spika kitaamua, wabunge waliridhia na Spika akakubalina na uamuzi huo.
Wabunge wakati akiomba msamaha walikubaliana bila kupingwa na uamuzi wa kamati kuhusu Mbowe, Makonda, Mkuu wa Wilaya hata Bulaya, lakini walijikita katika kumwombea msamaha.
Mbowe anatuhumiwa kwamba katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa Saba wa Bunge Aprili 4, mwaka huu wakati unafanyika uchaguzi wa Wabunge wa Afrika Mashariki (AELA), alitoa kauli za dharau kwa mamlaka ya Spika.
Mbowe alizungumza na vyombo vya habari akisema “Spika amevunja Kanuni za Bunge, sheria hazikuheshimiwa, ubabe umetumika… ni mkakati wa kiserikali, tunajua Rais anahusika, Waziri Mkuu anahusika, viongozi wa chama chao wanahusika… tumeleta wagombea wazuri wawili, wamepigiwa kura za hapana kwa sababu ulikuwa ni mkakati wa CCM, tumeona ni ujinga na upumbavu mtupu”.
Mdee anatuhumiwa kwamba katika kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Saba wa Bunge kilichofanyika Aprili 4, mwaka huu, alifanya vitendo vya dharau kwa mamlaka ya Spika na akatoa lugha ya matusi, kuudhi na kudhalilisha bunge, kutokana na kosa hilo Kamati hiyo ilitoa adhabu ya kumsimamisha kuhudhuria vikao vya bunge.
Bulaya alishitakiwa kutokana na kitendo cha kuvuruga Bunge kwa kupiga makofi na kelele Mei 30, mwaka jana wakati wa kikao cha 32 wakati bunge likijadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Katika kika hicho, Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia aliomba mwongozo wa Spika kupitia kanuni ya 68 (7) akitaka kujua kwanini Serikali imewafukuza wanafunzi wa Diploma Maalum ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kutokana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kutokuwapo bungeni, Naibu Waziri wa Maji, Isaac Kamwelwe alisimama kujibu mwongozo wa Nasari aliyetaka bunge liahirishe kujadili bajeti hiyo kutokana na suala hilo la wanafunzi kufukuzwa ndani ya saa 24.
Kutokana na mwongozo huo, Naibu Spika hakuona kama utaratibu bora wa uendeshaji wa Bunge kuahirisha shughuli za bunge kwa jambo ambalo linashughulikiwa na serikali.
Ndipo baadhi ya wabunge waliomba mwongozo, huku wakipiga kelele na kugonga meza na kurusha vitabu hovyo na kukataa maekelezo ya Naibu Spika ya kuwataka wabunge akiwamo Ester Bulaya kuacha vurugu hizo ili naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji ahitimishe hoja.
Kutokana na vurugu hizo kuendelea kwa muda, Naibu Spika aliagiza Bulaya kutokana na kudharau Mamlaka ya Spika aliagiza afike mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Bulaya alifika mbele ya Kamati ya Bunge Aprili 20, mwaka huu akituhumiwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu na dharau kwa mamlaka ya Spika na akadhibitisha kwamba kweli alifanya na akaomba radhi.
Makonda anatuhumiwa kwamba Februari 2, mwaka huu, katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kuulizwa kuhusu kujuana, kutajana wenyewe na hatua gani zitachukuliwa akajibu, “… Zingine ni mbwembwe tu, unajua mle ndani wakati mwingine wanachoka na kusinzia lazima kuwe na watu kidogo akili zao zinawasaidia kuamka, kucheka na wafurahi maisha yanaendelea.”
Mnyeti anatuhumiwa kwa kuandika kwenye facebook kuhusu Februari 3, mwaka huu kuhusu changamoto zilizoainishwa kwenye kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Miitaa, kuhusu matumizi mabaya ya madaraka ya wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuwakamata na kuwaweka mahubusu wabunge, madiwani na watumishi wa umma.
Mnyeti aliandika, “Upuuzi mtupu. Wabunge hawa hawajielewi. Nawashauri fanyeni kazi zenu za wengine waachieni wenyewe.” Wabunge na viongozi hao waliitwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa wakati tofauti na wote walikiri makosa yao na kamati hiyo iliwasilisha ripoti na wabunge walijadili na kukuridhia kuwasamehe kutokana na kukiri makosa yao na kuomba radhi kwa kwa spika, bunge na wabunge.
Spika wa Bunge baada ya mtoa hoja, Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Almasi Maige alihitimisha hoja hizo kwa kusema walitoa adhabu hiyo kwa Mdee kutokana na kutoonesha dhamira ya dhati ya kuomba radhi lakini aliwachanganya wabunge kwa kuwaingiza katika imani za dini.
“Alituchanganya kwa kuweka neno la Mungu mbele, tukaamua kumpa adhabu ya kukaa nje bunge moja, adhabu ambayo ni ndogo kwa sababu alishawahi kusimamishwa mabunge mawili, lakini tumeshangaa, ndani ya Bunge alivyokuwa mlokole.
Tumepata taabu tumeshindwa kuandika upya adhabu yake baada ya kuomba radhi bungeni,lakini tunakubaliana na uamuzi wa bunge kutokana na ombi la wabunge kumwombea msamaha mbunge huyo na kuanza maisha mapya.
Wabunge wamwokoa Mdee Wabunge kwa umoja wao walisimama na kuomba adhabu ya kumsimamisha Mdee asihudhurie Bunge la Bajeti waliomba itenguliwe, wakiongozwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), ambaye aliomba mbunge huyo kwa sababu ameomba radhi na kukiri kwa adabu bungeni asamehewe kwa kosa hilo.
Selasini alisema kutokana na kitendo cha mbunge huyo kuomba radhi kwa kamati, kwa spika, Bunge na wapiga kura wake wa Kawe, Bunge liridhirie msamaha huo na kumsemehe.
Wabunge waliochangia akiwamo, Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Ngwali (CUF) alisema mtoto akinyea mkono haukatwi, hivyo anasimama nafasi ya mama kumwomba Spika, Naibu Waziri, Hamis Kigwangalla na wabunge wote, wamsamehe.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliomba kutokana na Mdee kuomba msamaha bungeni kwa kumtanguliza Mungu, Bunge limsamehe, lifungue ukurasa mpya na asirudie tena kufanya kosa hilo.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) alisema, wabunge wanatakiwa kulilinda bunge kwa kuheshimiana wabunge wenyewe na ndipo hata viongozi wengine wataliheshimu.
“Tumsamehe Mdee kwa sababu aliomba radhi kwenye kamati na mbele ya bunge kwa unyenyekevu mkubwa, tumsamehe na tulinde bunge kwa wivu mkubwa,” alisema. Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Abdallah Bulembo (CCM) alimpongeza Mbowe kwa kuwa mnyenyekevu mbele ya kamati, akasema waliobaki ni vijana Mdee, Bulaya, Makonda na Mnyeti, wajitahidi kuheshimu kiti cha spika na viongozi wa serikali waheshimu mhimili wa Bunge.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) alisema, Mdee alimeomba radhi kimtego, kwamba nitajitihidi kutorudia, Mungu ataniongoza, inaonesha kwamba kama anaweza kurudia tena.
Ghasia alisema, Spika ni kiongozi mkubwa bungeni, hivyo kumdharau yeye ni kuwadharau wabunge wote. Mbunge wa Ileje, Janeth Mbene (CCM) alisema wabunge ni kioo cha jamii, inatakiwa kuwa mfano, akasema Mdee anatakiwa kuomba msamaha bila masharti, na asirudie makosa hayo.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment