TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara imewafikisha mahakamani watu wanne akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri Wilaya ya Musoma, Karaine Kunei (64) kwa makosa mbalimbali ya rushwa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Takukuru Mkoa, Holle Makungu, washtakiwa wengine waliofikishwa mahakamani ni Magera Andrew (40), Ofisa Kilimo Msaidizi halmashauri hiyo na Pilly Mzita (53) ambaye alikuwa karani wa mahesabu katika Halmashauri ya Musoma na sasa yuko halmashauri ya Butiama.
Washtakiwa wamefikishwa mahakamani jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Musoma na kusomewa mashtaka na waendesha mashtaka wa Takukuru, William Fussi akisaidiana na Moses Malewo.
Katika mashitaka ya kwanza, upande wa mashtaka umedai kuwa Septemba 1, 2009, Andrew alitumia vibaya mamlaka yake kwa kuiwezesha Kampuni ya Winam General Traders kulipwa Sh 16,800,000 kinyume cha mkataba wa ukarabati wa lambo la Kisamwene.
Katika mashitaka ya pili upande wa mashtaka umedai kuwa Aprili 1, 2009, Andrew alitumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri wake kwamba Hemed Maftah alistahili kulipwa Sh 640,000 kwa huduma ya uhakiki na upimaji malambo Wilaya ya Musoma.
Katika mashitaka ya tatu upande wa mashtaka umedai kuwa Aprili 24, 2009 kuwa Kunei alitumia nyaraka za uongo kuonesha kuwa Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa, Maftah aliipa ushauri Halmashauri ya Musoma.
Katika mashitaka ya nne upande wa mashtaka umedai kuwa Septemba 11, 2009 kwa lengo la kumdanganya mwajiri Mzita aliandaa hundi ya malipo Sh 640,000 kwa wakala wa uchimbaji visima na mabwawa, Maftah.
Katika mashitaka ya tano upande wa mashtaka umedai kuwa Novemba, 2009 katika tarehe zisizofahamika Andrew akiwa na nia ovu ya kudanganya alifoji sahihi ya Maftah kuonesha ndiye aliyeandaa fomu ya kukamilisha mradi.
Mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Kunei amekana shtaka dhidi yake na washtakiwa wengine wawili hawakuwepo mahakamani.
Upande wa mashtaka umeiarifu mahakama kuwa uchunguzi wa shauri umekamilika na umeomba tarehe nyingine ya kutaja shauri kwa kuwa washtakiwa wengine hawakufika mahakamani na haukuwa na pingamizi dhidi ya dhamana ya mshtakiwa.
Kesi imeahirishwa hadi Aprili 28, mwaka huu itakapokuja kwa kutajwa na mshtakiwa yuko nje kwa dhamana ambapo amewasilisha hati ya nyumba yenye thamani isiyopungua Sh milioni 2.7 pamoja na wadhamini wawili waliosaini dhamana ya Sh milioni 2.4 kila mmoja.
0 Maoni:
Post a Comment