MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela mtu na mkewe baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kumiliki na kujihusisha na nyara za serikali za thamani ya Sh bilioni 2.2, kinyume na sheria.
Waliohukumiwa ni Peter Kabi (45) na mkewe Leonida Kabi (46) ambao walihifadhi meno ya tembo kwenye jeneza na kufunika na bendera ya Taifa kuonesha kuwa wanasafirisha msiba wa askari kwenda Tarakea.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambaye pia aliamuru vipande 212 vya meno ya tembo kukabidhiwa kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliwatia hatiani washitakiwa hao wiki iliyopita ambapo upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi na Elia Athanas waliomba kuongeza shahidi mmoja ili kukazia hukumu hiyo.
Mtafiti wa wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Emmanuel Lyimo (32) aliieleza mahakama kuwa wamekuwa wakifanya utafiti kujua hali halisi ya tembo nchini kupitia sensa mbalimbali.
Alidai kuwa 2012 walifanya sensa ya wanyamapori baada ya kuona kwamba tembo wanapungua kwa kasi kikubwa ambapo ilifikia asilimia 50.
Alidai mwaka 2006, kulikuwa na tembo 134,000 na baadaye 2009 walikuwa 100,000 na kwamba hadi kufikia 2012 idadi ya tembo ilipungua na kufikia 43,000.
“Baada ya kuona hali mbaya ya tembo katika mbuga zetu, serikali ikaandaa Operesheni Tokomeza mwaka 2013 kwani walipungua kufikia tembo asilimia 53.3, lakini baada ya kufanya doria idadi iliongezeka na kufikia tembo 50,000,” alidai Lyimo.
Alidai kuwa hutambua tembo waliouawa kwa ujangili au kwa njia ya kawaida kwa kuangalia idadi ya mizoga kwa kuwa tembo wanaokufa kwa njia ya ujangili, meno yake hayakutwi eneo la tukio.
Aliendelea kudai kuwa tembo ana faida nyingi katika masuala ya mazingira na uchumi na kwamba utafiti wao huufanya kwa kutumia ndege ambazo hufungwa kamera.
Akielezea athari za kuuawa kwa tembo, shahidi huyo alidai kuwa kuuawa kwa tembo 93 ni idadi kubwa kwani uzalishaji wao huchukua muda mrefu ambapo hubeba mimba kwa miezi 22 na hadi tembo aweze kukua na kuzaa huchukua miaka 12.
Alidai tembo ni wanyama muhimu kwani ni miongoni mwa wanyama watano wenye thamani kubwa duniani na wanapowindwa kijangili kupunguza mapato ya serikali.
Aidha, alidai kuendelea kupungua kwa tembo inasababisha nchi kuondolewa kwenye mashirika ya Kitaifa ambayo huusika na ulinzi wa dunia wa wanyama hao na kwamba huathiri uhusiano.
Alidai adhabu ya makosa hayo ni kifungo cha miaka 20 au 30 pamoja na faini inayoweza kuongezeka mara mbili ya thamani ya meno ya tembo waliyokutwa nayo washitakiwa.
Pia alidai tembo 93 waliouawa ni wengi na katika sera ya Taifa kuhusu vita dhidi ya ujangili na mauaji ya tembo, mahakama ni mdau ndani ya vita hiyo na haiwezi kufanikiwa bila mahakama na kwamba kuna athari ambazo zimeainishwa kiuchumi hivyo mahakama itoe adhabu kali.
Akielezea kuhusu adhabu, Wakili Kadushi alidai kifungu namba 11 cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, kinaelezea kuwa masharti ni lazima kwa mahakama kutaifisha nyara zinazohusika na kesi hiyo ikiwemo meno ya tembo na mifupa mitano ya tembo.
“Lazima kitu chochote kilichotumika kufanyika kwa kosa la jinai vitaifishwe ikiwemo nyumba ambayo mshitakiwa wa kwanza anamiliki na viwe chini ya Mkurugenzi wa Wanyamapori,’’ alidai Kadushi.
Wakili wa utetezi wa washitakiwa hao, Bernard Mkagwa aliiomba mahakama itoe adhabu bila kumkomoa mshitakiwa na kwamba lengo la adhabu ni kurekebisha.
Pia aliomba mahakama ifikirie kuwa mtuhumiwa ni mke na mume ambao wanawatoto wawili wanaosoma pamoja na wazazi wazee ambao wanawategemea.
“Watuhumiwa wana miaka zaidi ya 45 na umiliki wa nyumba unaoelezwa kwenye ushahidi haupo.
Tunaomba adhabu nafuu chini ya adhabu iliyowekwa kisheria,’’ alidai.
Hakimu Shaidi alisema kosa la kwanza katika kesi hiyo ni miaka 15 jela, kosa la pili na la tatu miaka 20 na adhabu inakwenda kwa pamoja.
Ilielezwa katika tarehe isiyofahamika kabla ya Oktoba 27, 2012 katika maeneo mbalimbali ndani ya jiji la Dar es Salaam na Iringa, kwa pamoja washitakiwa waliunda kundi la uhalifu kwa ajili ya kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 210 vya meno ya tembo bila kibali.
0 Maoni:
Post a Comment