Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu Dar es Salaam (ZPC), Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi
wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura, wamepelekewa barua za mwito za
kuwataka wafike Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo.
Viongozi
hao wamepelekewa mwito huo kutokana na kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa
na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe dhidi yao.
Mbowe
amefungua kesi hiyo kupinga Makonda kumtaja katika orodha yake ya
watuhumiwa 65 wanaojihusisha na dawa za kulevya katika awamu ya pili na
kumtaka afike katika Kituo Kikuu cha Polisi, Februari 10 mwaka huu, kwa
ajili ya mahojiano.
Katika
kesi hiyo Namba Moja ya Mwaka 2017, Mbowe pamoja na mambo mengine,
anapinga mamlaka ya RC kumkamata kwa kile anachokiita kudhalilisha watu.
Kesi
hiyo imepangwa kutajwa leo na itasikilizwa na jopo la majaji watatu,
Sekieti Kihiyo ambaye ni kiongozi wa jopo hilo, akisaidiana na Jaji
Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday.
Mbowe
anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu
wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume cha Katiba.
Aidha,
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, jana alifungua maombi mahakamani hapo
akipinga kusudio la Kamanda Sirro la kumkamata kama hatajisalimisha
katika kituo cha polisi kwa mahojiano.
Mahakama
hiyo imetoa hati za mwito wa kufika mahakamani hapo kwa wadaiwa hao
ambao ni Makonda, Sirro na Wambura. Hata hivyo, inadaiwa Kamanda Sirro
alikataa kupokea mwito huo akielekeza kuwa hati hiyo ya mwito ipelekwe
kwa Wambura.
Wadaiwa kukataa kusaini
Kwa
mujibu wa Ofisa wa mahakama, Yusuph Juma ambaye alipeleka mwito huo,
alidai kuwa baada ya kuelekezwa na Kamanda Sirro kuwa ampelekee mwito
huo Wambura, alipokwenda kwa Wambura, hakumkuta.
Juma alidai hati ya mwito wa mkuu wa mkoa alipoupeleka hakumkuta na kwamba wasaidizi wake nao walikataa kuusaini mwito huo.
Mwishoni
mwa wiki, Kamanda Sirro akizungumza na waandishi wa habari alimtaka
Mbowe ajisalimishe mwenyewe kituo cha Polisi na kwamba kama hatafanya
hivyo basi watamsaka popote alipo na kumtia mbaroni.
Katika
maombi hayo, Mbowe anaiomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma
yake ya kumtia mbaroni pamoja na mambo mengine akidai kuwa kuna kesi ya
kikatiba ambayo tayari ameifungua mahakamani hapo.
Katika
maombi hayo, Mbowe anaiomba mahakama hiyo pia itoe amri ya kuwazuia
kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba
Mahakama Kuu imwachie na polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi
yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.
Katika
kesi ya Msingi ya Kikatiba, Mbowe anapinga kitendo cha Polisi kumtaka
afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa.
Anadai
kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na
kumweka ndani mtu iko kinyume cha Katiba kwa madai kuwa ilitungwa
katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.
Anadai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha Katiba.
Mbowe
pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake
kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo
ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu
Mkazi.
Vile
vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa
kutoa amri hiyo basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni
pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.
0 Maoni:
Post a Comment